TAMKO LA HAKIELIMU KUHUSU UPANGAJI WA VIWANGO VYA ALAMA,
MATUMIZI YA ALAMA ENDELEVU YA MWANAFUNZI NA UFAULU
4 NOVEMBA 2013
Hivi karibuni serikali imetoa tamko kuhusu mfumo mpya wa
upangaji wa viwango vya alama, matumizi ya alama endelevu ya mwanafunzi na
ufaulu. HakiElimu na wadau wake imetafakari tamko hilo na kutoa maoni ya
yafuatayo:
1. Hatujatambua lengo la serikali kuleta mabadiliko
haya; hasa ikikumbukwa kuwa Tume ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mh. Mizengo Pinda
haijawahi kuweka bayana taarifa yake kuhusu sababu za wanafunzi kutofaulu
vizuri katika mitihani ya kumaliza kidato cha nne. Wajumbe wa Tume hiyo
wamekuwa wakitoa dondoo fupi fupi za matokeo ya kazi yao-kama vile Bungeni na
katika hadhira nyingine za kitaifa; bila kutoa ripoti yenyewe. Je, kwa
mabadiliko haya,wizara inataka kuwaaminisha Watanzania kwamba alama zilivyokuwa
zimepangiliwa hapo awali,ndiyo sababu kuu ya wanafunzi kutofaulu vizuri?
2. Wizara imeeleza kwenye tamko lake kwamba
imeshirikisha wadau mbalimbali katika kufikia uamuzi huo. Hata hivyo, katika
orodha ya wadau walioshirikishwa inaonekana bayana kuwa asasi za utetezi
hazikupewa nafasi. Baada ya kufanya mawasiliano na baadhi ya wadau wanaodaiwa
kushiriki,wenyewe wamekiri kuwa ingawa walishiriki mawazo yao hayakuzingatiwa
na hawakukubaliana kuhusu kushusha alama za ufaulu kufikia 20 kati ya 100.
3. Mpangilio wa alama zitakazotumika kuanzia mwaka huu
unaleta tafsiri ya ndani kuhusu nia ya wizara kubadilisha alama hizo. Tafsiri
hiyo ni kulazimisha kuona kwamba wanafunzi wachache zaidi wanapata daraja la 5
(ambalo limeanzishwa badala ya daraja sifuri); kukiwa na uwezekano wa kupunguza
wanafunzi wanaopata daraja hili kwa asilimia 2.2% ukilinganisha na utaratibu
uliotumika kwa matokeo ya mwaka 2012. Mpangilio huo mpya una uwezekano wa
kuongeza kundi la wanafunzi wanaopata daraja la tatu na la nne kwa asilimia
12.1% kuliko utaratibu uliotumika mwaka 2012. Hata hivyo, alama hizo mpya
zinaweza kupunguza uwezekano wa kupata daraja la kwanza na la pili kwa asilimia
11.9%. Serikali na wadau wengine wa elimu wanatambua bayana kuwa njia kuu ya
kuboresha elimu na matokeo katika mitihani ni kuboresha utaratibu wa utoaji wa
elimu. Kwa nini serikali, hasa katika kipindi hiki inataka kuona matokeo mazuri
bila kuwekeza kwenye mipango ya kuboresha mfumo na utaratibu wa utoaji wa
elimu? HakiElimu inatafsiri uamuzi huo wa serikali kama ni kukwepa ukweli na
utaalamu; na badala yake serikali inatafuta njia ya mkato ya kuwafurahisha
wazazi na wananchi ili wapunguze kelele.
4. Serikali imekubali kutumia asilimia 40 kutoka kwenye
Alama za Tathmini Endelevu ya Mwanafunzi (Continuous Assessment, CA), ili
ziunganishwe na alama 60 za mtihani wa mwisho. Hata hivyo, uzoefu unaonesha
kuwa alama hizo zilikuwa zinachakachuliwa huko shuleni, na hata Baraza la
Mitihani Tanzania mwaka huu walikiri hilo kutokea. Wizara ya Elimu na Mafunzo
ya Ufundi itatumia njia gani kuhakikisha kuwa zinapatikana alama sahihi toka
shuleni zinazoendana na uwezo wa mwanafunzi? Je, kwa kiasi gani walimu
wameandaliwa na kujengewa mazingira mazuri ya kufanikisha zoezi hili? Hata
hivyo, serikali inapaswa pia kuwaeleza watanzania uzoefu wa nchi nyingine za
Afrika katika matumizi ya alama za CA; wengine wanatumia asilimia ngapi? Ni
muhimu kuwa na ushahidi kuwa kiwango cha CA tutakachokitumia kitaboresha
utaratibu wa kutathmini wanafunzi; na kuwatendea haki badala ya kuwaghiribu au
kuwaumiza.
5. HakiElimu inasikitika kuona wizara inalazimisha kila
mwanafunzi atakayefanya mtihani wa kidato cha nne au cha sita awe amefaulu.
Hiyo inathibitishwa na tafsiri ya alama ambazo zitatumika zinazoonesha kwamba
kuanzia atakayepata alama sifuri mpaka mia moja atakuwa amefaulu kwa namna
fulani. Kwa mfano, hata atakayepata alama kuanzia 0 mpaka 19 katika somo fulani
atahesabiwa kuwa amefaulu, japo katika kiwango kisichoridhisha. Kwa nini wizara
inakosa ujasiri wa kukubali kuwa mwanafunzi atakayepata chini ya alama fulani
ahesabiwe kuwa hakufaulu?
6. Kwa upangaji huo mpya wa alama za ufaulu, Tanzania
itakuwa nchi ya kwanza katika bara la Afrika kwa kuwa na kiwango cha chini
kabisa cha ufaulu katika elimu ya sekondari na kuna hatari kwamba kushushwa kwa
alama za ufaulu kutapunguza ama kuondoa hamasa ya wanafunzi kusoma kwa bidii,
kwa kuamini kuwa hawatafeli na cheti watapata tu. Kama wadau wote tunakubaliana
kuwa nia ya kutoa elimu ni kuandaa Watanzania ambao watakuwa na maarifa na
uwezo wa kushindana na wengine wanaosoma katika nchi nyingine Afrika.
7. HakiElimu pia inasikitika kuona kuwa wizara
inapotosha malengo ya “Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now-BRN)” kwa kutafuta
njia za mkato. BRN imeeleza bayana kuwa kati ya mikakati itakayotumika kupata Matokeo
Makubwa katika elimu ni kuboresha mchakato wa kufundisha na kujifunza shuleni
na kuboresha utaratibu wa utoaji wa elimu kwa kuweka bayana majukumu ya Wizara
ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na ile ya TAMISEMI. Wizara iwaambie Watanzania
kuwa kwa kiasi gani upangaji huu wa alama utasaidia kuboresha mazingira ya
ufundishaji na ujifunzaji kwa maana ya kumjengengea mwalimu uwezo, mazingira
mazuri na hamasa ya kufundisha na pia kutengeneza mazingira mazuri ya
mwanafunzi kujifunza. Katika haya, je, ni kweli kwamba huu upangaji upya wa
madaraja ni kipaumbele chetu namba moja? Si busara kushughulikia mpangilio wa
alama na madaraja kwanza wakati mchakato wa kuboresha mfumo wa elimu ili kupata
hayo matokeo mazuri bado uko chini. Kitendo hicho ni kukurupuka na kuruka hatua
muhimu zinazoweza kuboresha elimu.
8. HakiElimu inawatahadharisha Watanzania, wakiwemo
wazazi, wanafunzi na vijana wenye nia ya kurudia mitihani ili wapate vyeti; na
serikali yenyewe kuzingatia ukweli kwamba: Elimu ni uwezo, SIYO cheti. Jitihada
za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi zinaonesha wazi kuwa nia ni kuona
matokeo mazuri hata kama matokeo hayo hayataendana na uwezo walio nao
wanafunzi. Katika kutengeneza raslimali watu ya kutosha, Tanzania kama ilivyo
kwa nchi nyingine haina namna ya kukwepa kuhakikisha kwamba mfumo wa elimu
unaandaa vijana au wananchi wenye uwezo wa kukabiliana na changamoto
zinazowakabili wao wenyewe, jamii na Taifa kwa ujumla; pia kuwa na wananchi
ambao watakuwa na ujasiri, tija na ubunifu, katika uzalishaji katika shughuli
na fursa mbalimbali watakazozipata au kuzitafuta. Hali hii haipatikani kwa
kuhangaika na alama za ufaulu kama kipaumbele. Tunahitaji kuhangaika na mfumo
wa utoaji elimu utakaotusaidia kuleta mapinduzi ya kweli ya kiuchumi, kijamii
na kisiasa.
HakiElimu inaishauri Serikali kusitisha matumizi ya
alama na madaraja haya mapya. Irudi kwa wadau na ushahidi kuhusu uamuzi huu;
huku ikitoa nafasi ya kuchukua maoni ambayo yanaweza kuboresha mfumo wa upimaji
wa wanafunzi. Wakati zoezi hilo linaendelea, HakiElimu inaisisitiza Serikali
kutumia matokeo ya tafiti mbalimbali na mipango iliyopo kushughulikia dosari na
changamoto zinazorudisha nyuma elimu yetu, hasa zile zinazokwamisha ufundishaji
na ujifunzaji shuleni.
Tamko hili limesainiwa na,
Elizabeth Missokia Mkurugenzi Mtendaji, HakiElimu

0 comments:
Post a Comment