TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
MKUTANO kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na viongozi wa vyama vya siasa vyenye
uwakilishi Bungeni umemalizika Ikulu, Dar Es Salaam, muda mfupi uliopita leo,
Jumanne, Oktoba 15, 2013 kwa pande hizo mbili kukubaliana kama ifuatavyo:
Moja , kwamba vyama vyote vya siasa nchini
vyenye mawazo, maoni na mapendekezo ya kuboresha Sheria ya Kurekebisha Sheria
ya Mabadiliko ya Katiba viwasilishe mapendekezo yao haraka Serikalini ili
ifatutwe namna ya kuyashirikisha mapendekezo hayo katika marekebisho ya Sheria
hiyo.
Pili, kwamba vyama vya siasa nchini, kama wadau
muhimu katika mchakato wa Katiba Mpya, viangalie namna ya kukutana na kujenga
mfumo wa mawasiliano na maridhiano wa jinsi kwa pamoja vitakavyosukuma mbele
mchakato huo kwa maslahi mapana ya nchi yao na mustakabali wa taifa. Kituo cha
Demokrasia Tanzania (TCD) kimepewa jukumu la kuratibu jambo
hilo ikiwa ni pamoja na kuandaa mkutano wa vyama hivyo na wadau wengine nchini.
Viongozi wa vyama vyama vya siasa waliokutana na
Mheshimiwa Rais Kikwete ni Mheshimiwa Profesa Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa
CUF; Mheshimiwa Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa CHADEMA na Mheshimiwa James Mbatia
ambaye ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi.
Wengine ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Mheshimiwa Philip
Mangula, Mheshimiwa Isaack Cheyo ambaye amemwakilisha Mwenyekiti wa Chama cha
UDP Mheshimiwa John Cheyo na Mheshimiwa Nancy Mrikaria ambaye amemwakilisha
Mwenyekiti wa TLP Mheshimiwa Augustine Mrema. Waheshimiwa John Cheyo na Mrema
wako nje ya nchi.
Wengine ambao wameambatana na wenyeviti wao ni
Mheshimiwa H. Mnyaa na Bwana Julius Mtatiro wa CUF, Waheshimiwa Tundu Lissu na
John Mnyika wa CHADEMA na Bwana Martin Mng’ongo wa NCCR-Mageuzi.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
15 Oktoba, 2013
0 comments:
Post a Comment