HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,
MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, KWA WANANCHI, TAREHE 4 OKTOBA, 2013
Ndugu Wananchi;
Namshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehma, kwa
kutujaalia uzima na kutuwezesha kumaliza mwezi Septemba salama na kuwasiliana
kwa kutumia utaratibu wetu huu mzuri. Naomba radhi kuzungumza nanyi siku ya leo
kwa sababu nilikuwa safari na nilirejea jioni ya tarehe 30 Septemba, 2013.
Awali nilifikiria nisiseme, nisubiri mwisho wa mwezi wa Oktoba. Lakini, baada
ya kupata taarifa ya yaliyojiri, nimeshauriwa na nimekubali angalau niyasemee
baadhi ya mambo huenda itasaidia. Niwieni radhi nisipoyasemea baadhi ya mambo
siyo kwa kuyapuuza, bali kwa kuepuka hotuba kuwa ndefu mno. Nitayatafutia
mahali pengine pa kuyasemea.
UHUSIANO NA RWANDA
Ndugu Wananchi;
Katika hotuba yangu ya mwisho wa mwezi wa Julai,
nilizungumzia hali ya uhusiano wetu na Rwanda kutokuwa mzuri na tatizo la
ujambazi na wahamiaji haramu katika Mikoa ya Kigoma, Geita na Kagera. Nafurahi
kusema kuwa kwa yote mawili kuna maendeleo ya kutia moyo.
Tarehe 5 Septemba, 2013, nilikutana na kuzungumza na
Mheshimiwa Rais Paul Kagame wa Rwanda mjini Kampala. Tuliitumia fursa ya
ushiriki wetu katika Mkutano wa Nchi za Maziwa Makuu kuzungumzia uhusiano baina
yetu na nchi zetu. Mazungumzo yalikuwa mazuri na sote tulikubaliana kuwa
yaliyopita si ndwele tugange yajayo. Kwa sababu hiyo tulielewana kuwa
tutengeneze mazingira yatakayosaidia kutuliza hali na kurudisha nchi zetu
katika uhusiano mwema kama ilivyokuwa siku zote. Nawaomba ndugu zangu hususan
wanasiasa, watumishi wa umma, wanahabari na wenye mitandao ya kijamii na blog
na wananchi kwa ujumla tusaidie kuimarisha uhusiano mwema baina ya Rwanda na
Tanzania na watu wake.
MAJAMBAZI NA WAHAMIAJI HARAMU
Ndugu Wananchi;
Katika hotuba hiyo pia nilisema kuwa tutachukua hatua
thabiti dhidi ya majambazi na wageni wanaoishi nchini bila ya kuzingatia
taratibu zinazohusika. Niliwataka majambazi wajisalimishe wao na silaha zao kwa
hiari. Wale wanaoishi nchini bila ya kuwa na kibali halali wahalalishe ukaazi
wao au warejee makwao. Nilitoa siku 14 kuanzia tarehe 29 Agosti, 2013 wafanye
hivyo kwani baada ya hapo tungeanzisha operesheni maalum ya kushughulika na
watu wa makundi yote mawili.
Ndugu Wananchi;
Kumekuwepo na mafanikio ya kutia moyo. Kwa upande wa
wahamiaji wanaoishi nchini kinyume cha sheria watu wapatao 21,254 waliondoka
kwa hiari. Hali kadhalika zaidi ya ng'ombe 8,000 waliondolewa na silaha 102
zilisalimishwa. Baada ya operesheni kuanza tarehe 6 Septemba, 2013 na
kumalizika tarehe 20 Septemba, 2013, wahamiaji haramu 12,828 walirejeshwa
makwao na watuhumiwa 279 wa unyang'anyi wa kutumia silaha walikamatwa. Aidha,
mabomu 10 ya kutupa kwa mkono (offensive hand grenades), silaha 80, risasi 780
na mitambo 2 ya kutengeneza magobole vilikamatwa. Pia, ng'ombe 8,226 walikamatwa
wakichungwa katika mapori ya hifadhi. Kwa upande wa mazao ya misitu, mbao 2,105
zilikamatwa pamoja na nyara mbalimbali za Serikali.
Ndugu Wananchi;
Agizo la kuwataka watu wanaoishi nchini isivyo halali
wahalalishe ukaazi wao au waondoke kwa hiari au wataondolewa lilipotoshwa hasa
na vyombo vya habari vya nje ya Tanzania. Walikuwa wanadai eti Tanzania ilikuwa
inafukuza wakimbizi. Madai hayo si ya kweli hata kidogo. Hadi kufikia tarehe 30
Septemba, 2013 wakimbizi 68,711 walikuwepo kwenye Kambi ya Nyarugusu, Mkoani
Kigoma. Hakuna mkimbizi ye yote aliyetakiwa kuondoka. Ukweli ni kwamba hakuna
mtu ye yote kati ya wale watu walioondoka kwa hiari au kusaidiwa kuondoka
wakati wa operesheni ambaye ni mkimbizi. Kama ingekuwa hivyo, wa kwanza
kulalamika wangekuwa wenzetu wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa.
Bahati nzuri jambo hilo halikutokea.
Ndugu Wananchi;
Yalikuwepo pia madai kwamba tunawaonea na kuwatesa watu
walioishi nchini miaka mingi. Ati iweje sasa ndiyo waambiwe kuwa siyo raia.
Siku zote Serikali ilikuwa wapi? Uraia haupatikani kwa kuishi nchi ya kigeni
kwa miaka mingi. Unapatikana kwa kutimiza masharti ya kuomba na kupewa uraia.
Kama mtu hakufanya hivyo anabaki kuwa raia wa nchi aliyotoka au walikotoka
wazazi wake. Ipo mifano ya watu mashuhuri ambao walilazimika kuachia nyadhifa
zao baada ya kugundulika kuwa siyo raia. Hawakuwa wanaonewa, ndiyo matakwa ya
Katiba na Sheria za nchi yetu.
Ndugu Wananchi;
Katika kutekeleza operesheni hii niliagiza kuwa wale
watu ambao wameishi hapa nchini miaka mingi ambao wana nyumba, mashamba au mali
mbalimbali au wameoa au kuolewa na wana watoto au hata wajukuu waelekezwe
kuhalalisha ukaazi wao. Iwapo watakataa kufanya hivyo basi wasaidiwe kurejea
kwao. Pia niliagiza watu wasiporwe mali zao wala kudhulumiwa. Sijapata taarifa
ya kufanyika kinyume na maelekezo yangu. Lakini kama wapo watu waliotendewa
tofauti, taarifa itolewe kwa Wakuu wa Wilaya na Mikoa au hata Ofisi ya Rais ili
hatua zipasazo zichukuliwe. Hatutaki watu wadhulumiwe au kuonewa.
Napenda kutumia nafasi hii kumpongeza Waziri wa Ulinzi
na JKT, Mheshimiwa Shamsi Vuai Nahodha na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mheshimiwa
Emmanuel Nchimbi kwa uongozi wao mzuri katika zoezi hili. Pia, nawapongeza
Makamanda na askari wa JWTZ na Polisi pamoja na maafisa wa Idara ya Uhamiaji,
Idara ya Mifugo, Idara ya Wanyamapori, Idara ya Misitu na Idara nyinginezo za
Serikali kwa kazi kubwa na nzuri waliyofanya. Najua awamu ya kwanza imeisha
tarehe 20 Septemba, 2013 na kama nilivyosema kuwa safari hii operesheni itakuwa
endelevu, muda si mrefu awamu ya pili itafuata. Nawaomba waendelee kuchapa kazi
kwa bidii, maarifa na nidhamu ya hali ya juu.
ZIARA YA CANADA NA MAREKANI
Ndugu Wananchi;
Kati ya tarehe 17 na 28 Septemba, 2013 nilifanya ziara
ya kikazi katika nchi za Canada na Marekani. Nchini Canada nilitembelea Chuo
Kikuu cha Guelph ambapo nilitunukiwa Shahada ya Heshima ya Uzamivu kwa kutambua
jitihada zetu tuzifanyazo kujiletea maendeleo na mafanikio ya kutia moyo
tunayoendelea kupata licha ya changamoto zinazotukabili. Katika mazungumzo
yangu na uongozi wa chuo hicho wamekubali kuwa na ushirikiano wa karibu na
Wizara zinazohusika na Elimu, Kilimo na Mifugo pamoja na Chuo Kikuu cha Kilimo
cha Sokoine, Morogoro na Chuo Kikuu cha Dodoma. Nimewataka Mawaziri wa Wizara
hizo na viongozi wa vyuo hivyo kuchangamkia fursa hiyo bila kuchelewa.
Ndugu Wananchi;
Nchini Marekani nilikutana na kuzungumza na maafisa na
viongozi mbalimbali wa Serikali ya nchi hiyo wakiwemo Rais Barack Obama na
baadhi ya Wabunge wa Bunge la Marekani. Mazungumzo yetu yalilenga kuimarisha
ushirikiano baina ya nchi zetu na mambo yalienda vizuri. Wote walituhakikishia
kuwa mambo tuliyoyazungumza na kukubaliana na Rais Barack Obama wakati wa ziara
yake nchini yanaendelea kufanyiwa kazi. Miongoni mwa hayo maombi yetu ya kupatiwa
vitabu milioni 2.4 vya sayansi na hisabati yamekubaliwa na utekelezaji umeanza.
Upatikanaji wa vitabu hivyo utamwezesha kila mwanafunzi wa sekondari kuwa na
kitabu chake.
Ndugu Wananchi;
Jambo lingine kubwa na la faraja kwetu ni kuwa
mapendekezo yetu ya miradi ya umeme na barabara za vijijini za kugharamiwa na
Serikali ya Marekani kupitia Shirika lao la Changamoto za Milenia yamepokelewa
vizuri. Kinachosubiriwa ni miradi ipi itakubaliwa na Bodi ya MCC na kiasi gani
cha fedha kitatengwa na Bunge la Marekani kwa ajili hiyo.
TUZO YA UHIFADHI
Jambo lingine muhimu katika safari yangu ya Marekani ni
kutunukiwa tuzo na "International Congressional Conservation
Foundation" kwa kutambua juhudi zetu katika kuhifadhi wanyama pori na
mafanikio tuliyoyapata. Licha ya changamoto mbalimbali tunazokabiliana nazo,
tuzo hii imetupa moyo wa kuongeza nguvu katika jitihada tunazozifanya sasa
kupambana na ujangili na matatizo mengine ya uhifadhi wa wanyama na misitu.
Ndugu Wananchi;
Kilichotupa moyo zaidi ni kauli za utayari wa kutusaidia
katika mapambano hayo zilizotolewa wakati wa kupewa tuzo na katika mkutano wa
mfuko wa Maendeleo wa Clinton na katika mkutano maalum wa kupambana na ujangili
na biashara ya meno ya tembo duniani.
BARAZA KUU LA UMOJA WA MATAIFA
Ndugu Wananchi;
Shabaha kuu ya safari yangu ya Marekani ilikuwa
kuhudhuria Mkutano wa 68 wa Umoja wa Mataifa unaoendelea jijini New York mpaka
Desemba, 2013. Mada kuu ya mkutano wa mwaka huu ni kuandaa agenda ya maendeleo
baada ya mwaka 2015 yaani: Post 2015 Development Agenda: Setting the Stage.
Kama mtakavyokumbuka Malengo ya Milenia yaliyoamuliwa na Baraza Kuu la Umoja wa
Mataifa mwaka 2000, yanafikia ukomo wa utekelezaji wake mwaka 2015.
Katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka huu mjadala
umehusu nini kifanyike baada ya mwaka 2015. Hata hivyo, mjadala huo unaanza kwa
kufanya tathmini ya utekelezaji wa yale Malengo Manane ya Milenia ya mwaka 2000
umefikia wapi mpaka sasa na utafikia wapi mwaka 2015 kwa kila nchi na kwa dunia
kwa ujumla. Tathmini ya jumla inaonesha kuwa kumekuwepo na jitihada kubwa ya
kutekeleza malengo haya katika kila nchi. Yapo malengo ambayo utekelezaji wake
umefikia shabaha hivi sasa na yapo ambayo upo uwezekano wa shabaha kufikiwa
ifikapo mwaka 2015. Vile vile yapo ambayo shabaha haitafikiwa.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wetu, Tanzania, tumefikia shabaha katika
mambo yafuatayo:
(1) Lengo la Milenia namba 2 kuhusu uandikishaji wa
watoto wenye umri wa kwenda shule ya msingi;
(2) Lengo la Milenia namba 3 hasa kuhusu usawa wa
kijinsia katika Shule za Msingi na Sekondari. Ukweli ni kwamba, wasichana
wanaanza kuwa wengi kuliko wavulana. Hatujafikia shabaha kwa upande wa usawa wa
kijinsia katika elimu ya juu na ni vigumu kulifikia ifikapo 2015. Pia
hatujafikia lengo kwa upande wa usawa wa Wabunge wanawake na wanaume. Hata
hivyo, kwa kutumia mchakato wa Katiba unaoendelea sasa tunaweza kufikia lengo
katika uchaguzi wa 2015 iwapo tutaamua iwe hivyo;
(3) Lengo la Milenia namba 4 kuhusu kupunguza idadi ya
vifo vya watoto wachanga na wale wenye umri chini ya miaka mitano;
(4) Tumefikia shabaha kwa Lengo la Milenia Namba 6
kuhusu kupunguza maambukizi ya UKIMWI; na
(5) Kwa upande wa lengo namba 7 kuhusu mazingira,
tumefikia shabaha kwa upande wa upatikanaji wa maji mijini. Bado tuko nyuma kwa
maji vijijini ingawaje tunaweza kufikia lengo ifikapo mwaka 2015 kama
tutaendeleza uwekezaji tulioamua kufanya katika bajeti ya mwaka huu. Lakini,
hatutaweza kufikia shabaha kwa upande wa usafi wa mazingira mijini na vijijini
ifikapo mwaka 2015. Safari bado ndefu sana.
Ndugu Wananchi;
Malengo ya Milenia namba 1 na namba 5 ambayo bado tuko
nyuma sana ya shabaha hatutafikia lengo ifikapo 2015. Tumeendelea kutekeleza
lengo la Milenia namba 1 kuhusu kupunguza umaskini na njaa kwa zaidi ya nusu
kutoka kiwango cha mwaka 2000. Hatua tunazochukua kuleta mageuzi katika kilimo
zina lengo la kuhakikisha usalama wa chakula na kuongeza mapato ya wakulima.
Mafanikio yanaanza kuonekana lakini si ya kiwango cha kutufikisha kwenye lengo
ifikapo mwaka 2015. Tunao, pia, mpango wa kupanua programu ya TASAF ya
Conditional Cash Transfer ili tuwafikie watu wengi maskini. Hata kama
tutafanikiwa kuutekeleza mapema mpango huu utatusogeza sana mbele lakini bado
tutakuwa chini ya lengo kwa upande wa kupunguza umaskini ifikapo 2015.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa Lengo la Milenia namba 5, kuhusu afya ya
kina mama wajawazito bado tuko nyuma katika kupunguza vifo vya kina mama
wajawazito na kuongeza idadi ya wajawazito wanaojifungua chini ya uangalizi wa
wataalamu wa afya. Hatutaweza kufikia shabaha ifikapo mwaka 2015. Mpango wa
Maendeleo ya Afya ya Msingi (2007 – 2017) una nia ya kukabiliana na matatizo
haya. Tumeongeza ujenzi wa zahanati, vituo vya afya na hospitali, tumeboresha
upatikanaji wa dawa na tumepanua sana mafunzo ya madaktari, wauguzi na wakunga
mambo ambayo yamesaidia kutufikisha hatua tuliyopiga mpaka sasa. Naamini juhudi
zetu tukiziendeleza zitatusogeza mbele zaidi ingawaje bado tutakuwa chini ya
lengo. Miaka michache ijayo, tatizo hili nalo litakuwa historia.
Ndugu Wananchi;
Lengo la Milenia namba 8 linazihusu nchi tajiri kuongeza
michango yao kusaidia nchi zinazoendelea kutekeleza Malengo ya Milenia. Bahati
mbaya sana mataifa tajiri hayajafikia viwango wanavyotarajiwa kutoa na hata
vile wanavyoahidi wenyewe kutoa katika majukwaa mbalimbali. Kama wangetimiza
ahadi zao, sura ya utekelezaji wa Malengo ya Milenia ingekuwa tofauti kabisa.
Ndugu Wananchi;
Hiyo ndiyo hali ya utekelezaji wa Malengo ya Milenia
hapa nchini. Hakuna nchi ye yote duniani iliyofanikiwa kutekeleza shabaha za
malengo yote kwa ukamilifu. Ushauri wa viongozi wote waliozungumza ulitaka
mataifa yaliyoendelea yatimize ahadi zao za kuchangia utekelezaji wa Malengo ya
Milenia. Ilionekana suala la upatikanaji wa fedha halina budi kuangaliwa kwa
makini sasa na baada ya mwaka 2015. Bila ya hivyo ufanisi utakuwa mdogo katika
kuongeza kasi ya utekelezaji kwa pale paliposalia kufikia malengo ya 2015 na
hata kwa Malengo ya baada ya mwaka 2015.
MASHAMBULIZI YA KIGAIDI YA WESTGATE, NAIROBI
Ndugu Wananchi;
Wakati nikiwa safarini, tarehe 21 Septemba, 2013
kulitokea shambulilizi la kigaidi katika Jengo la Biashara la Westgate, huko
Nairobi, Kenya. Watu 67 walipoteza maisha na zaidi ya 200 walijeruhiwa.
Nilituma salamu za pole na rambirambi kwa Mheshimiwa Rais Uhuru Kenyatta na
wananchi wa Kenya na kuwahakikishia kuwa tupo pamoja nao katika wakati huu wa
majonzi.
Nafahamu kuwa baada ya tukio hilo watu wengi hapa nchini
wameingiwa na hofu kuhusu usalama wetu. Ni hofu ya msingi kwani tarehe 8
Agosti, 1998 Ubalozi wa Marekani hapa nchini ulishambuliwa na magaidi na ndugu
zetu 11 wasio na hatia walipoteza maisha.
Ndugu Wananchi;
Napenda kuwafahamisha kuwa tangu shambulio la mwaka
1998, Serikali imekuwa inajenga uwezo wa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama
kupambana na ugaidi katika nyanja mbalimbali. Tunaendelea kujiimarisha bila
kusita siku hadi siku. JWTZ, Polisi na Idara ya Usalama wa Taifa wamekuwa na
ushirikiano wa karibu kwa ajili hiyo. Juhudi zetu hizo ndizo zinazotufanya tuwe
salama hadi sasa.
Baada ya tukio la Kenya, vyombo vyetu vya ulinzi na
usalama vimeimarisha mikakati yao maradufu. Pamoja na kujizatiti kwetu huko
hatuwezi kusema kuwa tukio la kigaidi halitaweza kutokea nchini. Uhakika huo
hatuna kwani hata mataifa makubwa na tajiri yameshambuliwa. Kilicho muhimu ni
kuendelea kuchukua tahadhari na wananchi kusaidia ili vyombo vyetu vifanikiwe
zaidi.
Hali kadhalika, tumewataka watu wote wenye shughuli
zinazokusanya watu wengi kama vile maduka, maofisi, mahoteli, migahawa n.k.
waweke kamera za ulinzi nje na ndani ya maeneo yao. Pia waangalie uwezekano wa
kuweka vifaa vya upekuzi (metal detectors and x-rays). Najua watu wanaweza
kulalamikia usumbufu au gharama, lakini gharama na hasara ya kushambuliwa ni
kubwa zaidi kuliko ya usumbufu huo.
Ndugu Wananchi;
Nawaomba muendelee kufanya shughuli zenu bila ya hofu
ingawaje msiache kuwa makini na kuchukua tahadhari. Watu watoe taarifa kwa
vyombo vya usalama wanapoona mtu au watu au kitu cha kutilia shaka. Ni muhimu
kwa usalama wake, wa kila mtu, jamii na taifa. Maafisa husika wa vyombo vya
ulinzi na usalama wataendelea kuelimisha umma kuhusu hatua mbalimbali za
tahadhari za kuchukua. Sisi Serikalini tumejipanga kuchukua hatua zaidi
kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi yetu na watu wake.
MCHAKATO WA KATIBA MPYA
Ndugu Wananchi;
Kama mtakavyokumbuka, Bunge lilitunga Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba Novemba, 2011. Sheria hii imeweka mchakato mzima wa kupata
Katiba hiyo na kuunda taasisi zake. Mwezi Mei, 2012, Tume ya Mabadiliko ya
Katiba iliundwa na imekamilisha hatua tatu muhimu katika mchakato huo. Hatua
hizo ni kupokea maoni ya wananchi, kutayarisha rasimu ya kwanza ya Katiba Mpya
na kupokea maoni ya Mabaraza ya Katiba ya Wilaya na ya taasisi. Hivi sasa Tume
inaandaa mapendekezo ya Rasimu ya Pili ya Katiba itakayopelekwa kwenye Bunge
Maalum. Baada ya tafakuri zake, Bunge Maalum litatoa rasimu ya mwisho ya Katiba
ambayo itapelekwa kwa wananchi kwa ajili ya uamuzi wa mwisho kupitia kura ya
maoni. Baada ya hatua hiyo, ndipo tutakapokuwa tumepata Katiba Mpya.
Ndugu Wananchi;
Baada ya Bunge la Novemba, 2011 kupitisha Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba, kulikuwepo na madai ya kutaka sheria hiyo iboreshwe
kutoka vyama vyote vya siasa vikiwemo vyama vya upinzani na Chama tawala.
Majadiliano yalifanyika baina ya Serikali na vyama hivyo pamoja na shirikisho
la asasi za kiraia. Makubaliano yalifikiwa kuwa marekebisho yafanyike kwa
awamu. Awamu ya kwanza ihusishe Tume ya Mabadiliko ya Katiba kisha hapo
yafanyike marekebisho yanayohusu Bunge Maalum na mwisho Kura ya Maoni.
Kama ilivyokuwa kwa mabadiliko yaliyohusu Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, safari hii nayo vyama vya siasa vilitoa mapendekezo yao.
Yalifanyika mazungumzo kati yao na Serikali na maelewano kufikiwa kuhusu maeneo
ya kufanyiwa marekebisho. Serikali ilitayarisha rasimu ya Muswada na kuuwasilisha
kwa wenzetu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Ndugu Wananchi;
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilitoa mapendekezo yake
na ushauri kwenye maeneo mawili. Kwanza kwamba uteuzi wa wajumbe wa Bunge
Maalum ufanywe na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushauriana na
kuafikiana na Rais wa Zanzibar. Pili walishauri kwamba kama Bunge Maalum
litashindwa kufikia maamuzi ndani ya siku 70 zilizopendekezwa, liweze kuongezwa
muda hadi kufikia siku 90. Maeneo mengine ya Muswada waliafikiana nayo.
Ndugu Wananchi;
Kwa kuzingatia utaratibu wa kutunga Sheria, Serikali
ilifikisha Muswada kwa Spika wa Bunge ambaye nae aliuwasilisha kwenye Kamati ya
Kudumu ya Katiba, Sheria na Utawala. Kama ilivyo ada, Kamati hiyo ilifanya
vikao na wadau na kupokea maoni yao kuhusu Muswada. Nimeambiwa kulikuwa na
mjadala wa kina na mapendekezo mazuri yalitolewa na wadau. Kisha hapo Wajumbe
wa Kamati walikaa wenyewe kujadili Muswada walikuwepo pia Wabunge ambao si
Wajumbe wa Kamati walioshiriki kwa vile Kanuni zinaruhusu. Nimeambiwa pia
kwamba mjadala ulikuwa mpana na wa kina zaidi. Mapendekezo kadhaa yalitolewa na
Wajumbe kuhusu vifungu mbalimbali vya Muswada.
Ndugu Wananchi;
Nimefahamishwa kuwa Wabunge wa vyama vyote walichangia
na kwamba baadhi ya nyakati mambo yalipokuwa ugumu mawazo mazuri ya baadhi ya
Wabunge wa upinzani yalisaidia kupata ufumbuzi. Nimeambiwa pia kwamba Wajumbe
wa Kamati na upande wa Serikali walikubaliana kwa maeneo mengi isipokuwa
machache ambayo walikubaliana kwa pamoja wayapeleke Bungeni ili Wabunge nao wayajadili
na kuyapatia ufumbuzi.
Ndugu Wananchi;
Baada ya Kamati kumaliza kazi yake, Waziri wa Katiba na
Sheria, Mheshimiwa Mathias Chikawe aliwasilisha Muswada Bungeni. Akafuatiwa na
Mheshimiwa Gosbert Blandes kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Katiba, Sheria na Utawala, kutoa maoni ya Kamati. Baadaye Msemaji wa Kambi
ya Upinzani, Mheshimiwa Tundu Lissu alitoa maoni yake.
Ndugu Zangu;
Baada ya watu hao watatu kutoa maoni yao ilitarajiwa
kuwa Wabunge wangeanza kujadili Muswada. Naambiwa mambo hayakuwa hivyo. Badala
yake kukazuka malumbano baina ya Spika na baadhi ya Wabunge wa Upinzani
wakitaka Muswada usijadiliwe. Ilifikia wakati hoja hiyo ikabidi iamuliwe kwa
kura ambapo ilishindwa. Katika hali isiyotarajiwa, Wabunge wote wa upinzani wakatoka
nje ya Bunge isipokuwa wawili. Kitendo hicho kimewanyima Wabunge wengi wa
upinzani fursa ya kutetea hoja zao walizozitoa kupitia hotuba ya Msemaji wa
Kambi ya Upinzani. Pia wamejinyima nafasi ya kusema mambo mengine wakati wa
mjadala na Kamati ya Bunge zima.
Wabunge waliokuwepo waliendelea kuujadili Muswada na
kutoa hoja na mapendekezo ya kuuboresha. Walifanya hivyo wakati wa mjadala na
wakati wa kupitia kifungu kwa kifungu. Baadhi ya hoja na mapendekezo
yalikubaliwa na mengine yalikataliwa. Miongoni mwa yaliyokubaliwa na Wabunge,
kwa mfano, ni kuhusu elimu ya mtu atakayekuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalum na
lile la ukomo wa uhai wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Ndugu Wananchi;
Kwa maoni yangu madai ya Kambi ya Upinzani
yanazungumzika na hata baadhi yangeweza kukubalika kama Wabunge wake
wangekuwepo Bungeni na kushiriki mchakato wote wa kujadili na kupitisha Miswada
Bungeni. Bahati mbaya hawakuwepo, hivyo hapakuwepo na mtu wa kusema mawazo yao.
Baada ya kupoteza fursa yao halali, kutaka kupata ufumbuzi nje ya Bunge ni
jambo lisilowezekana. Haya ni masuala yanayohusu Bunge ambayo hujadiliwa na
kuamuliwa Bungeni na si vinginevyo. Kuandamana nchi nzima au kuchukua hatua za
kutotii sheria kama Mwenyekiti wa CHADEMA, Mheshimiwa Freeman Mbowe anavyotaka,
hakutaleta mabadiliko wanayoyataka katika sheria hii. Naamini na wao
wanautambua ukweli huo.
Ndugu Wananchi;
Kuna msemo wa wahenga kuwa "historia
hujirudia". Naomba hekima ziwaongoze viongozi wa CHADEMA, CUF na
NCCR-Mageuzi na zituongoze sote kutumia utaratibu tulioutumia mwaka 2012.
Kulipotokea mazingira kama haya pande zote zilikaa pamoja na kuzungumzia hoja
moja baada ya nyingine na kukubaliana nini kifanyike na kifanyike vipi. Baada
ya kuridhiana hatua zipasazo za kisheria na kanuni zilichukuliwa na kumaliza mzozo.
Ndugu Wananchi;
Kufanya kinyume cha hayo hakutaleta ufumbuzi wa mzozo
huu. Tutaliingiza taifa kwenye matatizo yasiyokuwa ya lazima. Tukikataa kufanya
hayo Watanzania wanayo kila sababu ya kuhoji dhamira zetu na kutilia shaka nia
zetu. Watakuwa na haki ya kuuliza nia ni hii yetu sote ya kupata Katiba Mpya
kwa kutumia njia za kikatiba na kisheria au tuna dhamira nyingine iliyojifisha?
Kama dhamira yetu ni kutaka kupata Katiba mpya kwa
mujibu wa Katiba na Sheria, ushauri wangu na rai kwa ndugu zetu wa CHADEMA, CUF
na NCCR-Maguezi ni kuwa waachane na mipango ya maandamano na kufanya ghasia.
Badala yake watumie njia halali zinazotambulika kikatiba na kisheria kujenga
hoja za kufanya marekebisho wanayoyaona wao yanafaa kuboresha Sheria ya
Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Tukifanya hivyo tutakuwa
tunajenga badala ya kubomoa. Tutaliponya taifa. Sisi katika Serikali tuko
tayari.
Ndugu Wananchi;
Napenda pia kuzisemea baadhi ya hoja zilizotolewa na
Kambi ya Upinzani. Kwanza kabisa nasema kuwa nimesikitishwa sana na madai na
tuhuma za uongo eti katika uteuzi wa Tume ya Katiba sikuheshimu mapendekezo ya
TEC, CCT na walemavu.
Ndugu Zangu, Watanzania Wenzangu;
Siyo tu kauli hiyo ya Mheshimiwa Tundu Lissu ni uzushi
na uongo mtupu bali pia ni ya unafiki, fitina na uzandiki wa hali ya juu.
Nasema hivyo kwa sababu, sipendi kuamini kuwa Mheshimiwa Mbunge amesema yale
kwa kutokufahamu ukweli au kwa bahati mbaya. Amesema yale kwa makusudi mazima
ya kupotosha ukweli ili pengine isaidie kujenga hoja yake ya kutaka Rais
asiteue wale Wajumbe 166 wa Bunge Maalum.
Napenda ieleweke kuwa siishabikii kazi hiyo, lakini kwa
kutimiza wajibu na maslahi ya taifa nikiagizwa na Sheria za nchi nitafanya.
Nasema hivyo kwa sababu nafahamu ni kazi ngumu. Kama kazi ya uteuzi wa Wajumbe
30 wa Tume haikuwa rahisi hata kidogo, hii ya uteuzi wa watu 166 itakuwa ngumu
zaidi. Ile ya Tume ilikuwa ngumu kwa namna mbili. Kwanza, kwamba taasisi
zilizoomba na waombaji walikuwa wengi mno kuliko nafasi za kujaza yaani 15
Zanzibar na 15 Bara. Zanzibar ziliomba taasisi zaidi ya 60 na waombaji walikuwa
zaidi ya 200 wakati Bara kulikuwa na taasisi zaidi ya 170 zikiwa na waombaji
zaidi ya 500. Kupata watu 30 kutoka orodha kubwa kiasi hicho si mtihani mdogo.
Pili kwamba tulitakiwa kuunda Tume inayoasili sura ya taifa, yaani watu wa nchi
yetu kwa maeneo, vyama vya siasa, dini, wanawake, vijana, walemavu,
wafanyakazi, wasomi, Wabunge, Wawakilishi, wanasheria, wafanyabiashara,
wakulima, asasi za kiraia n.k.
Ndugu Wananchi;
Pamoja na changamoto hizo, lakini tulifanikiwa kuunda
Tume iliyopokelewa vizuri na jamii na kufanya watu wengi hata wale ambao
hawakuteuliwa wahisi kuwakilishwa. Tulifanyaje? Kwanza kabisa tulihakikisha
kuwa tunapata wawakilishi wa vyama vya siasa vyenye wawakilishi Bungeni na
kwenye Baraza la Wawakilishi na tunapata wawakilishi wa mashirika ya dini zetu
kubwa yaani, TEC, CCT na BAKWATA. Ndiyo maana nikasema kuwa kwa Mheshimiwa
Tundu Lisu kudai kuwa mapendekezo ya TEC na CCT hayakuheshimiwa ni uongo wa mchana
usiokuwa na kichwa wala miguu.
Baada ya hapo ndipo tukaangalia waombaji wa makundi na
taasisi nyingine. Tulijitahidi sana kupata watu ambao wanawakilisha kundi zaidi
ya moja. Tulifikiria hivyo kwa sababu ni ukweli ulio wazi kuwa si kila taasisi
iliyoomba itapata mwakilishi kwani hata tungependa iwe hivyo nafasi hazikuwepo.
Kwa kutumia utaratibu huu makundi mengi yamepata uwakilishi kutokana na watu
waliopendekezwa na makundi mengi. Tumefanya kazi kubwa sana ya kuwianisha mambo
na makundi ya maslahi mbalimbali nchini.
Ndiyo maana naiona mantiki ya Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania akishirikiana na Rais wa Zanzibar wa kuwateua Wajumbe wa
Bunge Maalum. Dhana kuwa kila kikundi kiteue chenyewe watu ingefaa sana kama
kungekuwepo na nafasi za kutosha kila kundi nchini. Hilo haliwezekani, labda
tuwe na Bunge Maalum lisilokuwa na ukomo wa wajumbe.
Ndugu Wananchi;
Mimi na Rais wa Zanzibar tumekuwa tunajiuliza baada ya
kazi ngumu na nzuri tuliyoifanya na iliyopongezwa na wengi ya kuteua Tume ya
Mabadiliko ya Katiba nini kilichoharibika sasa hata tuonekane hatuaminiki
kuteua hawa 166? Kama ni kwa sababu za Mheshimiwa Tundu Lissu, nimeshasema
hazina ukweli wowote. Ninapojiuliza kwa nini aseme uongo nashindwa kupata jibu
linaloingia akilini. Wakati mwingine nafikiria kuwa ni hiana. Lakini nadhani ni
hila za kisiasa zenye nia ya kutaka kupata watu wa kutetea maslahi ya chama
chake. Kama hiyo ndiyo shabaha basi amekosea sana.
Ndugu Zangu, Watanzania Wenzangu;
Hatutengenezi Katiba ya Chama fulani bali Katiba ya
nchi, Katiba ya watu wa vyama vyote na wasiokuwa na vyama ambao ndiyo wengi
kuliko wote. Lazima tuongozwe na ukweli huo na tuwe na msimamo huo wakati wote.
Lazima tukumbuke kuwa si watu wote wanaostahili au kuwa na sifa ambao wataomba
na kupata nafasi ya kuwa Wajumbe, hivyo wale wachache watakao bahatika lazima
wawasemee wote. Wanatakiwa kusikiliza na kuwakilisha mawazo ya wote hata wale
wasiokuwa wa Chama chao au kundi lao.
Ndugu Wananchi;
Bahati nzuri hii ndiyo sifa kubwa iliyooneshwa na
Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Wamewasimamia na kuwasemea watu wote
bila ya kubagua. Natambua kuwepo kwa baadhi ya watu ambao hawafurahii msimamo
huo na matokeo ya kazi yao. Watu hao kuwalaumu Wajumbe wa Tume kwa ajili hiyo
ni kuwaonea na kutowatendea haki. Tunataka watakaokuwa Wajumbe wa Bunge Maalum
nao waige mfano huu mzuri. Wajali maslahi mapana ya taifa letu na watu wake
badala ya kujali yale ya taasisi zao au makundi yao.
ZANZIBAR KUTOKUSHIRIKISHWA
Ndugu Wanachi;
Nimeambiwa pia kuliwepo madai ya Zanzibar kutokushirikishwa
ipasavyo. Nimeeleza kwa kiasi gani Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
imeshirikishwa na kutoa maoni yake yaliyojumuishwa katika Muswada. Hivyo basi
napata tabu kuyaelewa madai kwamba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
haikushirikishwa msingi wake nini! Labda kuna kitu sikuambiwa!
Nimeulizia kuhusu hoja ya Kamati kutokufanya vikao
Zanzibar kusikiliza maoni ya wadau wa Zanzibar. Nimeambiwa kuwa Kanuni za Bunge
hazina sharti hilo hivyo Kamati haistahili kulaumiwa. Kama hivyo, nashauri kuwa
suala hili lirudishwe Bungeni ili Wabunge walizungumze na kulifanyia uamuzi
muafaka. Vinginevyo watu wataendelea kulauminiana isivyostahili. Hivyo basi,
kuligeuza jambo hili kuwa ni suala la kukataa Muswada au kususia vikao vya
Bunge au kufanya maandamano sidhani kama ni sawa.
Ndugu Wananchi;
Nimeambiwa pia kuwa kulikuwa na hoja ya kutaka idadi ya
Wajumbe wa kutoka Tanzania Bara na Zanzibar iwe sawa kama ilivyo kwenye Tume ya
Mabadiliko ya Katiba. Sababu ya idadi ya Wajumbe wa Tume kuwa sawa inatokana na
utaratibu wao wa kufikia uamuzi. Ni kwa maelewano ya wote (consensus) na siyo
kwa kupiga kura. Ndiyo maana idadi imewekwa sawa ili sauti za pande zote
zisikike sawia. Bunge Maalum lina sharti la kufanya uamuzi kwa theluthi mbili
ya kura za kila upande kukubali. Bila ya hivyo hakuna uamuzi.
Hivyo basi, katika Bunge Maalum nguvu si uwingi wa kura
ambazo upande fulani unaweza kupata bali ni ulinganifu sawa wa kura za kila
upande peke yake. Huu ndiyo msingi unaotumika katika Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania hivi sasa kwa lengo la kulinda maslahi ya Zanzibar.
Zanzibar ina Majimbo 50 ya uchaguzi na Tanzania Bara ina Majimbo 189, hivyo
ukiamua kwa wingi kila wakati Wazanzibari watashindwa. Lakini, hapajakuwepo
madai ya Zanzibar nao kutaka kuwa na idadi sawa ya majimbo kama Bara au
kupunguza majimbo ya Bara yawe sawa na ya Zanzibar kwa sababu wingi si hoja.
Msingi unaotumika ni kutoa nguvu sawa za uamuzi kwa kila upande wa Muungano
wakati wa kuamua masuala ya Katiba. Hakuna mdogo wala mkubwa, wote wako sawa.
Hakuna mdogo kumezwa na mkubwa. Ndiyo msingi unaopendekezwa kutumika kwenye
Bunge Maalum hivyo hakuna kitakachoharibika kwa idadi ya Wajumbe
kutokukulingana. Nadhani inafaa ibaki ilivyo. Lakini kama Wabunge wataamua
waongeze idadi itakuwa kwa sababu nyingine siyo hii ya mfano wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba.
Ndugu Wananchi;
Katika orodha ya madai ya ndugu zetu wa upinzani lipo
suala la uhai wa Tume ya Katiba. Wanataka usiishe wanapokabidhi rasimu ya pili
kwa Bunge Maalum bali waendelee kuwepo mpaka mwisho wa mchakato. Nimeulizia
ilikuwaje? Nimeelezwa kuwa jambo hili halitokani na mapendekezo ya Serikali
wala ya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala. Limetokana na pendekezo
la Mbunge katika Bunge wakati wa kupitia vifungu na kuungwa mkono na Wabunge
wengi. Kwa hiyo kuilaumu Serikali si haki. Serikali inaweza kuwa mshirika
katika hoja hii.
Nami naiona hoja ya Wajumbe wa Tume kuwa na wajibu
wakati wa Bunge Maalum hasa wa kusaidia kufafanua mapendekezo ya Tume. Je
ushiriki huo uwe vipi? Je ni Wajumbe wote au baadhi yao ni jambo linaloweza
kujadiliwa.
Ndugu Wananchi;
Naomba nimalizie kwa kuwasihi viongozi wa CHADEMA, CUF
na NCCR-Mageuzi kuongozwa na hekima iliyotumika wakati tulipokuwa na tatizo
linalofana na hili kuhusu Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Mimi naamini kama
iliwezekana kufanikisha mambo wakati ule inaweza kufanya hivyo hata safari hii.
Itatufikisha pale tunapopataka salama salimini bila maandamano, kushupaliana au
uvunjifu wa amani. Kupanga ni kuchagua, naomba sote, mmoja mmoja na kwa umoja
wetu tuchague njia ya mazungumzo na maelewano kwani itaihakikishia nchi yetu
amani, usalama na utulivu. Tukifanya hivyo historia itatuhukumu kwa wema.
Mungu Ibariki Tanzania. Nawashukuru sana kwa
kunisikiliza.
0 comments:
Post a Comment