TANZANIA YAWAONYA WAASI WA M23





WAASI wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wa M23 wameonywa wasithubutu kuingia nchini kishari kwani wakifanya hivyo cha moto watakiona.

Lakini wanapaswa pia kujua kwamba kamwe Tanzania haitatishwa na kauli zao kwani nchi iko imara dhidi ya adui yeyote. Onyo hilo lilitolewa jana bungeni na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.

Waziri Membe alitaka waasi hao waache kutumia jila la Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kuifundisha Tanzania dhana ya wema ni nini.

Pamoja na kuwaagiza kuacha kutishia Watanzania, Waziri Membe aliwataka kuacha kubaka na kuua wananchi wa Kongo, vinginevyo Tanzania kwa kusaidiana na mataifa mengine chini ya uongozi wa Umoja wa Mataifa (UN) itaingia nchini humo kulinda wananchi.

Alisema ghasia zinazofanyika Kongo ‘zinazaa’ wakimbizi na kusema ni wajibu wa Tanzania ikishirikiana na mataifa mengine kulinda uhai wa wananchi wa Kongo.

Waziri Membe alisema hayo alipochangia makadirio ya matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) iliyopitishwa na Bunge jana huku akisaidia kujibu hoja za Wapinzani kuhusu M23 na usalama wa mpaka wa Ziwa Nyasa.

Waziri wa Ulinzi na JKT, Shamsi Vuai Nahodha katika hotuba yake alisema mipaka ya nchi kwa ujumla iko swari ingawa upinzani ulihoji kauli ya M23 na kujitoa kwa Malawi katika mazungumzo ya mgogoro wa mpaka.

Wizara ya Ulinzi na JKT jana ilipitishiwa na Bunge jumla ya Sh trilioni 1.1 ambazo kati yake sh bilioni 857.4 ni kwa matumizi ya kawaida n ash bilioni 245.6 ni kwa matumizi ya maendeleo.

Membe alisema Tanzania imepata baraka zote za kutoa kikosi cha Jeshi kwenda Kongo kuungana na majeshi mengine kulinda amani nchini humo, hivyo vitisho vilivyotolewa hivi karbuni havina masingi.

“Muda umefika kwenda kusaidia majirani zetu ili kuhakikisha Wakongo wanaishi kwa amani na kufanya shughuli zao na hakuna wa kututisha na kuzuia majeshi yetu kwenda Kongo,” alisema Waziri Membe.

Membe alisema amepokea barua kutoka kikundi hicho kikitishia kuwa endapo Tanzania itatoa askari wake kwenda nchini humo watauawa kwa mauaji ya halaiki.

“Nimepokea barua imetumwa kwangu ikiwa na anuani ya Mungu, inadai imetoka kwa Mungu, lakini lugha ndiyo hiyo hiyo tunayoisoma kila siku, huku ikimnukuu marehemu Baba wa Taifa kuwa binadamu wote ni sawa,” alisema.

“Nadhani walitaka kutumia jina la Mungu ili Serikali itishike na kushindwa kufanya majukumu yake. M23 wametutisha kama alivyotutisha Kanali Bakari wa Comoro kuwa vijana wetu wakienda pale watakuwa chakula cha mambo.

“Vijana walikwenda na badala ya kuwa chakula cha mambo wao wakala samaki na siku ya tatu Kanali Bakari alikimbia akivalia baibui na kuiacha nchi… vitisho vya M23 ni vya mtu ambaye amekata tamaa,” alisema.

“Hawa watu hawawezi kutumia jina la Baba yetu wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kutufundisha sisi juu ya wema ni nini, huku wakiendelea kuua watu na kubaka huku wakidalilisha wazee wao, huko kukufuru ni lazima tutakwenda kukomesha hilo,” alisisitiza huku akiwa na uso wa hasira.

Membe alisema endapo Jeshi la Tanzania litakwenda nchini humo kisha kuguswa na kikundi hicho, Tanzania itajibu mapigo.

Waziri huyo alisema endapo kikundi hicho hakipendi jeshi la Tanzania kwenda nchini humo, ni lazima wafanye mambo kadhaa ikiwamo kurudi katika mazungumzo ya Uganda, kuacha kuua raia wasio na hatia na kubaka na kujisalimisha kwa hiari.

CHANZO: Habari Leo
Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment