Kauli Kamili Ya Serikali Kuhusu Kufuta Matokeo Hii Hapa

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge),
William Lukuvi,
KAULI YA SERIKALI BUNGENI KUHUSU TAARIFA
YA AWALI YA TUME YA TAIFA YA KUCHUNGUZA MATOKEO
YA MTIHANI WA TAIFA WA KIDATO CHA NNE MWAKA 2012
UTANGULIZI



1. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni ya 49(1) ya Kanuni za
Kudumu za Bunge, Toleo la mwaka 2007, naomba kuwasilisha Taarifa ya
Awali ya Tume ya Taifa ya kuchunguza matokeo ya Mtihani wa Taifa wa
Kidato cha Nne mwaka 2012.
2. Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge watakumbuka kuwa
Matokeo ya Mitihani ya Kidato cha Nne mwaka 2012 yalionesha kuwa
kiwango cha ufaulu kimeshuka kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na miaka
ya hivi karibuni. Matokeo yaliyotangazwa mwezi Februari, 2012 yalionesha
kwamba kati ya Wanafunzi 367,756 waliofanya mtihani huo, Watahiniwa
126,847 ndio waliofaulu. Katika idadi hii, Wanafunzi waliofaulu katika Daraja
la Kwanza hadi la Tatu ni 23,520, sawa na Asilimia 6.4 na Daraja la Nne ni
103,327, sawa na Asilimia 28.1. Watahiniwa 240,909, sawa na Asilimia
65.5 ya Wanafunzi wote waliofanya Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2012
walipata Daraja la Sifuri.
3. Mheshimiwa Spika, kushuka kwa kiwango cha ufaulu kulihusu shule
za aina zote, yaani Sekondari za Serikali ikijumuisha zilizojengwa kwa nguvu
za Wananchi, Shule Binafsi na Seminari. Takwimu zinaonyesha kwamba
ukilinganisha matokeo ya Kidato cha Nne mwaka 2011 na mwaka 2012, Shule
za Wananchi matokeo yao yameshuka kwa Asilimia 1.82; Shule za Umma za
zamani (Kongwe) yameshukwa kwa Asilimia 6.43; Shule Binafsi yameshuka
kwa Asilimia 6.39; na kwa Shule za Seminari yameshuka kwa Asilimia 7.29.
Hali hii inaonyesha kwamba, matokeo katika Shule za Wananchi
yameshuka kwa kiwango kidogo ikilinganishwa na yale ya Shule za
Umma za zamani (Kongwe), Shule Binafsi na Shule za Seminari
ambazo zilitegemewa kufanya vizuri zaidi ya zile za Wananchi ambazo
matokeo yao yameshuka zaidi kwa kati ya Asilimia 6.4 na 7.3.
4. Mheshimiwa Spika, kutokana na matokeo hayo yasiyoridhisha na
ambayo yapo nje kabisa ya mwenendo wa ufaulu kwa miaka ya karibuni,
Serikali iliamua kuunda Tume ya Kuchunguza Kushuka kwa Kiwango cha
Ufaulu wa Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne mwaka 2012 kwa madhumuni
ya kupata ufumbuzi wa kudumu.
HADIDU ZA REJEA
5. Mheshimiwa Spika, Tume ya Uchunguzi ilipewa Hadidu za Rejea
zikiwemo zifuatazo:
i. Kubainisha sababu za matokeo mabaya ya Mtihani wa Kidato cha
Nne mwaka 2012;
ii. Kubaini sababu za kushuka kwa kiwango cha ufaulu katika
mitihani ya Kidato cha Nne mwaka 2011 hadi 2012;

iii. Kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukua kukabiliana na tatizo
la mwenendo wa kushuka kwa kiwango cha elimu mara moja,
kipindi cha muda mfupi, kati na kipindi cha muda mrefu;
iv. Kutathmini nafasi ya Halmashauri katika kusimamia Elimu ya
Sekondari katika Halmashauri zake;
v. Kuanisha sababu nyingine zinazoweza kuwa zimechangia hali hii
ya matokeo.
6. Mheshimiwa Spika, katika kutafakari Hadidu za Rejea hizo, Tume
imejikita katika kujibu Maswali Makuu matatu.
i) Kwa nini matokeo ya Kidato cha Nne kuanzia mwaka 2008
yamekuwa na mserereko wa kushuka kuliko miaka iliyotangulia?
ii) Kwa nini Wanafunzi wa Kidato cha Nne wa mwaka 2012 matokeo
yao yalikuwa mabaya kuliko ya wenzao wa mwaka 2011 pamoja
na kwamba ufaulu ulishuka tangu mwaka 2008? na
iii) Nini kifanyike.
WAJUMBE WA TUME YA UCHUNGUZI
5. Mheshimiwa Spika, Tume ya Uchunguzi iliongozwa na Prof. Sifuni
Mchome kutoka Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania na ndiye alikuwa Mwenyekiti.
Wajumbe wengine waliteuliwa kutoka Vyuo vya Elimu ya Juu, Baraza la
Wawakilishi, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Madhehebu ya Dini, Chama cha Walimu, Muungano wa wenye
Shule Binafsi na Muungano wa Walimu wa Sekondari. Orodha ya Wajumbe wa
Tume hiyo ni kama ifuatavyo:
NA. JINA TAASISI
ANAYOTOKA
NAFASI
1. Prof. Sifuni Ernest Mchome Tume ya Vyuo Vikuu
Tanzania
Mwenyekiti wa
Tume
2. Mhe. Bernadeta K. Mushashu
(Mb.)
Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa
Tanzania
Makamu
Mwenyekiti
3. Mhe. Abdul J. Marombwa
(Mb.)
Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa
Tanzania
Mjumbe
4. Mhe. Suleiman H. Hamisi
(MBLW)
Baraza la Wawakilishi
Zanzibar
Mjumbe
5. Mwalimu Honoratha
Chitanda
Chama cha Walimu
Tanzania (CWT)
Mjumbe
6. Ndugu Rakesh Rajani TWAWEZA Mjumbe
7. Mwalimu Daina W. Matemu Umoja wa Wakuu wa
Shule za Sekondari
Tanzania
Mjumbe
8. Mwalimu Kizito Innocent Taasisi ya Elimu Mjumbe

Lawa Tanzania
9. Mwalimu Mabruki J. Makame Baraza la Elimu
Zanzibar
Mjumbe
10. Prof. Mwajabu K. Possi Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam
Mjumbe
11. Mwalimu Nurdin Mohamed Chuo cha Ualimu cha
Al-Harmain
Mjumbe
12. Ndugu Peter Maduki Baraza la Kikristo la
Huduma za Jamii
Mjumbe
13. Ndugu Mahmoud A. K.
Mringo
Chama wa Wamiliki
na Mameneja wa
Shule na Vyuo Visivyo
vya Serikali
Mjumbe
14. Ndugu Abdallah H. Mohamed Chuo Kikuu cha Taifa
Zanzibar
Mjumbe
TAARIFA YA TUME YA UCHUNGUZI
6. Mheshimiwa Spika, tarehe 28 Aprili, 2013 Tume ya Uchunguzi wa
Matokeo ya Kidato cha Nne mwaka 2012 ilikamilisha kazi yake katika Awamu
ya Kwanza na kutoa Taarifa ya Awali. Uchambuzi wa Taarifa hiyo ya awali
unaonesha kuwa kutokana na Uchunguzi uliofanyika, kwa muhtasari Tume
imebaini mambo muhimu yafuatayo:
6.1 Matokeo ya Kidato cha Nne kuanzia mwaka 2008 yamekuwa na
mserereko wa kushuka kuliko miaka iliyotangulia kwa sababu
mbalimbali ikiwemo changamoto zinazotokana na mafanikio yaliyopo
sasa ya kuongezeka sana kwa Idadi ya Shule za Msingi na za Sekondari,
hususan kati ya mwaka 2001 na sasa (2013); na hivyo kuwa na idadi
kubwa ya Wanafunzi waliopo Shuleni.
Kwa mfano, katika kipindi cha mwaka 1961 hadi 2001 Idadi ya
Wanafunzi wa Shule za Msingi imeongezeka kutoka Wanafunzi 486,470
(1961) hadi 4,875,764 mwaka 2001, sawa na ongezeko la Wanafunzi
4,389,294 katika kipindi hicho cha takriban miaka 40. Hata hivyo, kati
ya mwaka 2001 hadi 2012 Wanafunzi wameongezeka kutoka
4,875,764 mwaka 2001 hadi 8,247,472 mwaka 2012, sawa na
ongezeko la Wanafunzi 3,371,708 katika kipindi cha takriban miaka 11
na hivyo kufanya jumla ya Wanafunzi wote wa Shule za Msingi kuwa
8,247,472 mwaka 2012.
Kuhusu Shule za Sekondari Idadi ya Wanafunzi imeongezeka kutoka
11,832 mwaka 1961 hadi 289,699 mwaka 2001 ambayo ni sawa na
ongezeko la Wanafunzi 274,867 katika kipindi hicho cha miaka 40.
Lakini kati ya mwaka 2001 hadi 2012 Idadi ya Wanafunzi imeongezeka
kutoka 289,699 (mwaka 2001) hadi 1,884,270 mwaka 2012, sawa na
ongezeko la Wanafunzi 1,594,571 katika kipindi cha miaka 11 tu.
Juhudi hizi zimetokana na Mipango mbalimbali iliyoandaliwa chini ya Mpango
wa Maendeleo ya Sekta ya Elimu wa mwaka 1999. Mipango hii ni pamoja na:
1. Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) wa mwaka 2002
ambapo:

a) MMEM I ambayo ililenga katika kufungua Shule zaidi ili
Wanafunzi wengi wa rika lengwa waweze kujiunga na Elimu ya
Msingi;
b) MMEM II ambayo ililenga katika kuboresha ubora wa elimu
itolewayo katika Shule za Elimu ya Msingi; na
c) MMEM III ambayo ililenga katika kuendelea kuimarisha ubora wa
Elimu ya Msingi baada ya mafanikio ya MMEM I na MMEM II.
2. Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES) wa mwaka 2004
ambapo:
a) MMES I ambayo ililenga katika kufungua Shule zaidi za Sekondari
katika ngazi ya Kata ili Wanafunzi wengi zaidi wanaomaliza Elimu
ya Msingi waweze kujiunga na Elimu ya Sekondari Kidato cha
Kwanza; na
b) MMES II ambayo ililenga katika kuendelea kuimarisha ubora wa
Elimu ya Sekondari kadri Idadi ya Wanafunzi wa Elimu ya
Sekondari wanavyoendelea kuongezeka.
Changamoto zinazoambatana na mafanikio haya ni pamoja na
mazingira yasiyoridhisha ya kufundishia na kujifunzia, ikiwemo
upungufu wa miundombinu muhimu ya shule kama vile Madarasa,
Maabara, Madawati, Maktaba, Nyumba za Walimu, Hosteli na majengo
mengine muhimu ya Shule. Vilevile, kuna tatizo la uhaba wa Walimu,
Vitabu, zana za kufundishia na matatizo ya Ukaguzi wa Shule. Vilevile,
Tume imebaini kuwa Mfumo wa Elimu ya Msingi na Sekondari
unakabiliwa na changamoto nyingine mbalimbali ambazo Taifa inapitia
kwa sasa ikiwemo masuala ya Kisera, Kisheria, Kimfumo, Kimuundo
pamoja na changamoto za uhaba wa Rasilimali Fedha na Rasilimali
Watu. Tume inaendelea kufanyia kazi maeneo haya kwa kushirikiana na
Wataalamu na Wadau wengine;
6.2 Kuhusu matokeo ya Kidato cha Nne mwaka 2012, Tume imebaini
kwamba, pamoja na Wanafunzi hawa kuwa katika mazingira
yanayofanana na ya wenzao wa miaka iliyopita na kwamba ufanisi
katika shule kwa ujumla umekuwa unashuka kwa sababu mbalimbali,
ufaulu wao umeshuka zaidi kwa sababu ya mabadiliko ya mchakato wa
kuandaa na kutoa matokeo ya mtihani kwa mwaka 2012. Mfumo
uliotumika mwaka 2012 katika kupanga matokeo na madaraja ni tofauti
na ule uliotumika mwaka 2011 na miaka iliyotangulia. Uchunguzi
unaonesha kuwa mwaka 2011, Baraza la Taifa la Mitihani lilikuwa
linachakata Alama za mwisho kwa kutumia mfumo ambao
ulikuwa unabadilika kutegemea hali ya ufaulu wa Mwanafunzi
ambao ni “National Mean Difference” (NMD). Utaratibu huu ulitokana na
tofauti ya Wastani wa Kitaifa wa Alama za Maendeleo kutoka Alama za
Maendeleo Endelevu (Continued Assessment – CA) za Watahiniwa wote
na Wastani wa Kitaifa wa ufaulu wa Mitihani ya mwisho kwa somo
husika. Kila Mtahiniwa aliongezewa “National Mean Difference”
iliyokokotolewa katika Alama za Mtihani wa mwisho ili kupata Alama

itakayotumika kupata Daraja la ufaulu. Kimsingi, kila somo lilikuwa na
NMD yake kulingana na Continued Assessment (CA) zilivyo kwa mwaka
husika.
Lakini mwaka 2012 Baraza lilitumia Mfumo Mpya ambao ulikuwa
haubadiliki kutegemea hali ya ufaulu wa Mwanafunzi, yaani kuwa na
Viwango Maalum vya Kutunuku (Fixed Grade Ranges). Tume imebaini
kwamba, pamoja na kwamba Mfumo huo uliandaliwa kwa nia nzuri,
Utaratibu huo mpya haukufanyiwa utafiti na maandalizi ya kutosha
kabla ya kutumika.
MAPENDEKEZO YA AWALI YA TUME
7. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia masuala mbalimbali yaliyojitokeza
wakati wa uchunguzi, Tume katika Taarifa yake ya awali imetoa
mapendekezo mbalimbali yakiwemo yale yanayohitaji kutekelezwa kwa
haraka. Kutokana na kuwepo kwa mapendekezo hayo ambayo inabidi
yafanyike kwa haraka, tarehe 29 Aprili, 2013 Baraza la Mawaziri lilipokea
Taarifa ya Awali ya Tume na kuijadili ambapo liliridhia mapendekezo hayo
yaanze kutekelezwa mara moja. Maamuzi hayo ya Baraza la Mawaziri
yanalenga kutenda haki kwa Walimu na Wanafunzi ambao juhudi zao za
kufundisha na kujifunza zimepimwa kwa kutumia Mfumo mpya ambao
hawakupata fursa ya kushirikishwa na kuandaliwa. Mapendekezo hayo ni
yafuatayo:
i. Matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2012 yafutwe na
yaandaliwe upya kwa kutumia utaratibu uliotumika mwaka
2011;
ii. Standardisation ifanyike ili matokeo ya Wanafunzi yalingane na
juhudi walizoziweka katika kusoma kwa mazingira na hali halisi ya
Tanzania na uamuzi wa Taifa kuongeza idadi ya Shule na
Wanafunzi wakati uwekezaji katika ubora unaendelea;
iii. Baraza la Taifa la Mitihani limeelekezwa kuzingatia kuwa pamoja
na kwamba Sheria ya kuanzishwa kwake inawaruhusu kufanya
marekebisho ya mchakato wa mitihani, lakini marekebisho yoyote
ya kubadilisha Utaratibu wa kupanga viwango vya ufaulu na
madaraja ya matokeo ya Mitihani, lazima yahusishe Wadau
wote wanaohusika na Mitaala, Ufundishaji na Mitihani.
Wakati Tume inaendelea kukamilisha kazi yake, uamuzi wa
Baraza la Taifa la Mitihani wa kutumia utaratibu mpya wa
kupanga viwango vya ufaulu na madaraja ya matokeo ya Mitihani
uliotumika mwaka 2012 usitishwe na badala yake Baraza la
Mitihani litumie Utaratibu wa mwaka 2011 kwa Kidato cha Nne na
cha Sita kwa Mitihani yote ukiwemo utaratibu wa Standardization
na kutoa Matokeo mapya kwa kuzingatia maelekezo haya.
Aidha, mchakato wa Mfumo wa Tuzo wa Taifa (National
Qualifications Framework) na Mfumo wa kutahiniwa/kutathmini
maendeleo ya Mwanafunzi katika masomo yake (National
Assessment Framework) ukamilishwe haraka iwezekanavyo.

UTEKELEZAJI WA MAPENDEKEZO YA TUME
8. Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu wa mapendekezo hayo,
Baraza la Mawaziri limeamua kwamba utekelezaji wa mapendekezo hayo
uanze mara moja.
9. Mheshimiwa Spika, Tume ya Uchunguzi itaendelea kukamilisha
Taarifa yake vizuri kwa kuhusisha Wadau mbalimbali ili kupata maoni zaidi na
ushauri wao juu ya mambo mbalimbali yaliyobainika wakati wa uchunguzi
kabla ya kuikamilisha na kuitoa kwa matumizi ya Umma na Vyombo
mbalimbali.
HITIMISHO
10. Mheshimiwa Spika, Serikali inaipongeza sana Tume kwa kutoa
mapendekezo ya awali ambayo Serikali imeyaridhia. Aidha, Serikali
inawashukuru Wananchi wote na Wadau mbalimbali wa Sekta ya Elimu
wanaoendelea kutoa maoni na ushauri wao kwa Tume.
11. Mheshimiwa Spika, Serikali inawahakikishia Wananchi kuwa
itaendelea kuboresha Elimu Nchini ili kuwezesha Watoto wetu wapate
mafanikio katika maisha na maendeleo yao, kwani Wahenga wanasema
“Elimu ni Ufunguo wa Maisha”.
12. Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment