Dk. Slaa, Kabwe ‘waumana’

Dr Slaa-Katibu Mkuu Wa Chadema(kushoto) Na Zitto Kabwe Mbungu Wa
Kigoma Kusini(Kulia)
Na Esther Mbussi

HATUA ya Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Wilbrod Slaa, kukanusha kupitia mitandao ya kijamii tukio la kunusurika kuuawa kwa bastola, Shida Salum, mama mzazi wa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, limeiibua familia na kumuonya aache kuingilia mambo yanayoihusu.

Onyo hilo limetolewa na msemaji wa familia ya Kabwe, Salum Kabwe, ambaye ni mtoto mkubwa wa kiume wa Shida Salum, ikiwa ni takribani wiki moja sasa baada ya gazeti hili kuripoti tukio hilo.

Shida Salum, alivamiwa nyumbani kwake Tabata Bima, Ijumaa ya Aprili 19, mwaka huu na vijana wawili waliokuwa wakitaka kompyuta yake ndogo, (laptop), simu yake ya mkononi na flashi.

Baada ya tukio hilo, aliripoti katika Kituo cha Polisi cha Tabata na kupewa RB ya TAB/RB/2898/2013/TAARIFA, kabla hajaelekezwa kwenda kutoa taarifa katika Kituo cha Polisi Buguruni, ambako alipewa RB, BUG/RB/5113/13, kutishia kuua kwa bastola.

Dk. Slaa, baada ya kusoma gazeti hili toleo la Jumatano iliyopita, ambalo liliipa uzito mkubwa habari hiyo, alidai kuwa aliwasiliana na mama Zitto ili kujua ukweli wa kilichompata, lakini alimpa majibu yaliyotofautiana na habari iliyondikwa na MTANZANIA Jumatano.

Hatua hiyo ilimsukuma kuandika ujumbe wa kukanusha habari hiyo katika mtandao wa kijamii wa Jamii Forum na andishi lake hilo lilisomeka hivi; “Baada ya kusoma gazeti la MTANZANIA kwa nafasi yangu ya Katibu Mkuu nilimpigia simu Mama Zitto, kwanza kumpa pole na pili kujua hasa yaliyomsibu.

“Aliyoniambia mama Zitto yanapingana na yote yaliyoandikwa humo, mengine yakidhaniwa yamesemwa na mama Zitto na mengine yakiandikwa na wachangiaji kwa hisia kali, ni hatari sana kwa taifa.

“Sikuishia hapo, nikatafuta mfumo wangu wa kiuongozi na chombo chetu cha usalama nikapata jibu langu. Nimeongea na ofisa wangu, Sabula, kinachozungumzwa hapa ni kinyume kabisa na alichozungumza na mama Zitto na nimethibitisha hayo kwa mama Zitto mwenyewe.

“Nimewasiliana na viongozi wangu wa Jimbo na Kata, kuhusiana na kijiwe chochote kinachojengwa na taarifa sahihi ni kuwa hakuna kijiwe chochote kinachojengwa na kilichoombewa fedha kwa mama Zitto.

“Ila kuna Ofisi ya Kata inakarabatiwa ndiyo iliyoombewa fedha na wahusika walifika kwa mama Zitto na wakapewa fedha Sh. 30,000.”

MTANZANIA Jumatano lilipowasiliana na mama Zitto ili kujua ukweli wa kauli za Dk. Slaa, alisema baada ya taarifa ya kuvamiwa kwake na kunusurika kuuawa kuchapishwa na gazeti hili, Dk. Slaa alimpigia simu na kumuuliza kilichotokea kwenye gazeti.

Alisema alimsimulia mwenendo wa tukio na hata alivyohojiwa na waandishi wa gazeti hili na yeye (Dk. Slaa) alidai kuwa atatoa maelekezo kwa Sabula kufuatilia jambo hilo kwa sababu yuko jimboni kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda, hivyo akirudi wangewasiliana.

Hata hivyo, hadi alipokuwa akihojiwa alisema hajamuona Sabula wala hajawasiliana naye.

“Nashangaa baada ya hapo amekuwa msemaji wa polisi, mimi sijamgusa kwa lolote, yeye anaongea nini? Namheshimu sitaki malumbano naye, aache polisi wafanye kazi yao. Anawatuma watu JF (Jamii Forums), waandike uongo, hivi mimi kweli naweza kujisingizia jambo kubwa kama hili, ili iweje, na kwa faida ya nani? Namuacha awe msemaji wa familia yangu kama ameamua kufanya hivyo,” alisema mama Zitto.

Naye msemaji wa familia ya Kabwe, Salum alipozungumza na MTANZANIA Jumatano kuhusu mwenendo huo, alisema familia yake inakasirishwa na mambo yanayoendelea kwenye mitandao ya kijamii kuhusu kuvamiwa kwa mama yao na kuonya kuwa wanaofanya hivyo waache mara moja.

Alisema familia yake imeshangazwa kusikia watu wanasema tukio hilo limetengenezwa na kuhoji kuwa inawezekanaje mtu wa aina ya mama yake atengeneze kifo.

“Haya mambo waache polisi wafanye kazi yao, sitaki na sipendi hiki kitu kifanywe kama mtaji wa kisiasa, maana hata sisi wenyewe hatujui tatizo ni nini ndiyo maana tumeiachia polisi. Nawaonya wanasiasa kuepuka kusema lolote kuhusu suala la kuvamiwa kwa mama yetu, familia haijamtuma mtu yeyote kuwa msemaji wa familia kuhusu suala la usalama wa mama yetu.

“Tunalaani kitendo chochote kuhusu maisha ya mama yetu kuingiliwa na wanasiasa, hatutavumilia kwa namna yoyote ile kuingiliwa katika jambo hili, suala hili lipo polisi na tuache polisi wafanye uchunguzi wao,” alisema Salum.

“Ukiangalia kundi linalotukana na kuongea maneno ya ajabu katika mitandao siku zote ni hao hao, hivi mtu anaweza kutunga tatizo, akienda kwenye safari zake anaonekana kama anaenda kumnadi mwanae, sisi kama familia inatuuma sana.

“Siku chache kabla ya tukio, Katibu (Dk. Slaa) alipomtuma Sabula kuja nyumbani wakati huo akiwa Mbeya, kuna mtu kutoka Mbeya alinitumia ujumbe kwenye simu yangu ya mkononi akinieleza kuwa kuna mtu ametumwa kuja kwa mama kupeleleza, niwe makini,” alisema.

Alifafanua kwa kueleza kuwa Sabula ni mtu mwenye matatizo na kutoa mfano wa tukio la kukamatwa kwa aliyekuwa mwanachama wa Chadema, Habib Mchange, siku za nyuma, ambapo yeye (Salum) alikwenda polisi kujua tatizo lililosababisha awekwe korokoroni, akiwa kituoni hapo alimuona Sabula lakini hata hivyo alijificha.

Alisema baada ya kumkimbia polisi, alikwenda kuandika barua kwa Dk. Slaa akieleza kuwa Salum anamsaidia Mchange polisi, jambo ambalo lilimshangaza kwa sababu hakujua maana hasa ya hatua hiyo ya Sabula.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa kipolisi Ilala, Marietha Minangi, alipoulizwa hatua iliyofikiwa na ofisi yake kuhusu upelelezi wa kesi hiyo, alikwepa kuzungumzia suala hilo, kwa kueleza kuwa yuko kwenye kikao, hivyo apigiwe baadaye, lakini alipopigiwa tena hakupokea simu na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno licha ya kuonyesha kuwa umepokelewa katika simu yake, hakuujibu.
CHANZO:MTANZANIA
Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment