CUF yatishia kujitoa Katiba Mpya

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimeanika uamuzi wake wa baraza kuu la uongozi huku kikiionya Serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuhuwu mchakato wa Katiba mpya na uchaguzi mdogo wa jimbo la Chambani. CUF kimetangaza kusudio la kujitoa katika mchakato wa katiba na kuuungana na taasisi, vyama na baadhi ya Watanzania ambao wamekwisha kuonyesha shaka juu ya mchakato huo.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahimu Lipumba alikuwa akizungumzia maazimio matano ya kikoa cha baraza kuu la uongozi wa chama hicho kilichokaa kwa siku mbili na kumalizika juzi usiku.

Profesa Lipumba alidai Dar es Salaam jana kuwa chama hicho hakijaona nia njema na utayari wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya kuleta katiba iliyozingatia maoni ya wananchi bali ni maagizo ya CCM kwa manufaa ya wachache.

“Tunasubiri rasimu itolewe na kuisoma lakini tayari tunajua yaliyomo ni maagizo ya CCM na CUF tunaishangaa tume ya Jaji mstaafu, Joseph Warioba kushindwa kujijengea historia ya maisha yao katika siasa na kuendelea kukumbukwa kwa wema kupitia katiba hii.

“CUF hakitakuwa tayari kuiunga mkono katiba ambayo haitakuwa na misingi imara ya demokrasia na isiyotokana na maoni ya Watanzania… tutakuwa tayari kuwahamasisha wananchi nchi nzima kuikataa katiba ya maagizo ya CCM.

“Hatupo tayari kuona matumizi makubwa ya gharama za kuukamilisha mchakato ambao kimsingi ni kiini macho. Tunataka rasimu itolewa na kuwekwa hadharani ili wananchi watoe maoni yao kabla haijapelekwa bungeni kupoigiwa kura.

“CUF tuna ushahidi juu ya watu walioingizwa katika mabaraza ya katiba ngazi ya kata na ndiyo maana yamekuwapo malalamiko mengi, tutaungana na wale waliotangulia kuonyesha shaka wakiwamo Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA) na Chadema wanaosubiria hiyo rasimu,”alisema.

Profesa Lipumba alisema katiba mpya inayotokana na wananchi wenyewe itasaidia kujenga dira mpya ya mabadiliko ya uchumi, siasa, muundo wa uendeshaji wa nchi na kuongeza uwajibikaji kwa viongozi.

Alisema ikiwa tume italeta katiba ya kikundi cha watu wachache na wenye dhamana na kuilazimisha kuwa katiba mpya itasababisha taifa kukosa utulivu.

Uchaguzi Chambani

Profesa Lipumba alisema pia kuwa CUF kimemteua Yusuph Salum Hussein kuwa mgombea ubunge jimbo la Chambani-Pemba katika uchaguzi mdogo utakaofanyika Juni 16, mwaka huu.

Profesa Lipumba alisema Hussein ni miongoni mwa wanachama 12 waliochukua fomu kuwania nafasi hiyo iliyoachwa wazi kutokana na kifo cha Salim Hemed aliyefariki dunia ghafla akiwa katika shughuli za bunge.

Alisema baraza kuu la CUF limeiagiza kamati ya utendaji na maandalizi ya uchaguzi wa ndani ya chama kuhakikisha uchaguzi huo unaratibiwa vizuri viongozi makini waweze kupatikana kwa ngazi zote ambao wataweka mikakati ya ushindi 2015.

Maagizo serikalini

Profesa Lipumba alisema CUF kimegundua nchi ipo katika matatizo makubwa ya mfumo katika kuasisi asasi zitakazojenga demokrasia na kuendeleza uchumi wa kisasa.

“Kutokana na hali hiyo, tunaiomba Serikali kutekeleza miradi ya maendeleo, kuonyesha nidhamu ya matumizi ya fedha za umma, iache utaratibu wa kukopa bila kuwa na mkakati wa matumizi mazuri.

“Serikali iache utaratibu wa malipo kwa mfumo wa stakabadhi ghalani, iache vitendo vya unyanyasaji, dhuluma, ifanye uchunguzi wa matukio ya mashambulio ya viongozi wa dini na madhehebu.

“Itumie busara kutatua mpasuko wa dini unaonekana kuendelea kukua kwa kasi na kuleta chuki na uhasama, kutafuta suluhisho la nani anastahili kuchinja na Serikali ya CCM iwe na utaratibu wa kutoa taarifa sahihi na wakati,”alisema.

Alisema Serikali inapaswa kuhakikisha inaboresha daftari la kudumu la wapiga kura katika kuelekea uchaguzi mkuu 2015.

Kuhusu matokeo mabaya ya kidato cha nne mwaka 2012, alisema ni vema Baraza la Mtihani Tanzania (NECTA) likafumuliwa na kusukwa upya kwa kuwa viongozi waliopewa dhamana ya kuliongoza na kamati zake wamedhihirisha wapo kwa maslahi ya posho tu.

Profesa Lipumba aliitaka Serikali ya CCM kuondokana na ubabaishaji wa kushughulikia sekta ya elimu nchini kwa vile ni hatari kwa kizazi kijacho na uhai wa taifa.
CHANZO:MTANZANIA
Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment