Bomu Jingine Kanisani Dar.

TAHARUKI ya ugaidi ilizuka jijini Dar es Salaam jana, baada ya taarifa kuzagaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii kuwa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Mtongani Kunduchi limelipuliwa kwa bomu lililorushwa. Taarifa hizo zilieleza kuwa, bomu hilo lilirushwa usawa wa kanisa hilo na kusababisha watu kutaharuki kutokana na kishindo kikubwa kilichosikika.
Hata hivyo, akizungumzia tukio hilo ofisini kwake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Charles Kenyela, alikiri bomu hilo kurushwa karibu na kanisa hilo, lakini alisema kuwa lilipigwa na askari waliokuwa katika doria ya kawaida, kufuatia taarifa walizozipata za kuwepo kwa wahalifu karibu na kanisa hilo.

Kenyela alisema Jeshi la Polisi lilipata taarifa kuwa wahalifu hao walikuwa wakiweka kijiwe katika eneo la nyumba iliyo jirani na kanisa hilo ambayo walikuwa wakiitumia kucheza kamari, kuvuta bangi na kisha kufanya vitendo vya uhalifu, ikiwemo uporaji.

“Uvumi huo si wa kweli, askari wakiwa katika kazi za kawaida walifika Mtongani, kuna nyumba ya ghorofa ambayo haikaliwi na watu, awali kulikuwa na taarifa za kuwapo vijana wakicheza kamari, kuvuta bangi, jioni wanafanya uhalifu, hivyo kulikuwa hakuna njia mbadala ya kuwakamata zaidi ya kupiga bomu,” alisema Kenyela.

Alisema kufuatia bomu hilo lililopigwa hewani, walijitokeza na kukimbilia sehemu mbalimbali, ikiwemo kando ya eneo la bahari pamoja na kanisani.

Kenyela alisema polisi walipata ushirikiano kutoka kwa waumini pamoja na wananchi waliokuwa eneo hilo na hivyo kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa sita katika hekaheka hizo.

Aliwataja watuhumiwa waliokamatwa kuwa ni Hussein Sadick (18), ambaye hana kazi, Nasri Kajembe (25), Kasim Seif (21), ambaye ni kondakta, Juma Khatibu (17) mwanafunzi kidato cha 4 Boko Sekondari, Japhet Nicodemus (20) na mtoto David Gereza (13) ambao wote ni wakazi wa Mtongani Kunduchi.

Katika kamata kamata hiyo, Kamanda Kenyela alisema walifanikiwa kukamata vifaa kama nondo, vyuma na misokoto ya bangi ambavyo wamekuwa wakitumia watuhumiwa.

Kamanda Kenyela alipotakiwa kufafanua ni kwa nini hawakutoa tahadhari mapema kwa wananchi badala ya kuwashtukiza kwa bomu hilo, alisema kuna matukio ambayo njia za kawaida zinashindikana kutumika, hivyo kuamua kutumia njia nyingine mbadala, ikiwemo kama hiyo.

Kamanda Kenyela aliwapa pole wananchi waliopatwa na mshtuko wa bomu hilo, ambapo alisema kwa sasa lazima kuwa na taharuki kunapotokea kishindo cha bomu, kufuatia tukio la hivi karibuni jijini Arusha.

Bomu hilo lililopigwa eneo la kanisa liliibua taharuki kubwa kwa wakazi wa Dar es Salaam, hasa kutokana na kwamba zimepita siku sita tangu litokee tukio lenye sura ya ugaidi, baada ya mtu mmoja kurusha bomu katika Kanisa la Parokia ya Mtakatifu Joseph Mfanyakazi Olasiti, Jijini Arusha.

Janga hilo la aina yake lilitokea wakati Balozi wa Baba Mtakatifu nchini, Askofu Mkuu Francisck Padilla na Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki Arusha, Josephat Lebulu wakiwa kwenye shughuli ya uzinduzi wa Parokia mpya ya Olasiti.

Watu watatu waliuawa huku wengine zaidi ya 60 wakijeruhiwa kufuatia tukio hilo, ambalo tayari watu 12 wamekamatwa kwa ajili ya mahojiano.
CHANZO:MTANZANIA
Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment