Mufti Smba Aunda Timu Kujadli Udini

MGOGORO wa kidini unaoendelea kufukuta nchini unazidi kuchukua sura mpya, baada ya Mufti wa Tanzania, Sheikh Issa bin Shaaban Simba, kuunda timu ya masheikh kujadili suala hilo. Timu hiyo ya masheikh ambayo inatarajiwa kuanza kazi muda wowote kuanzia sasa, itaungana na viongozi wa dini ya Kikristo kwa ajili ya kujadili namna ya kudumisha amani nchini.

Wakati Mufti akifanya hivyo, Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi, ameonesha wasi wasi wake na kusema kuwa migogoro ya kidini inayotokea nchini huenda imegubikwa na msukumo wa wanasiasa waliobeba ajenda ya siri.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uhusiano) Stephen Wassira, amewafananisha watu wanaochezea amani ya nchi na wendawazimu na kuonya juu ya mchezo huo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mufti Simba alisema uamuzi wa kuunda timu hiyo umetokana na utashi na dhamira njema kwa taifa.

“Katika wazo la kuunda timu hii nimezingatia zaidi suala la maslahi ya ujirani mwema, amani na usalama wetu sote katika kulinda na kudumisha uhuru kwa kuabudu hapa nchini.

“Ninatambua kwamba sisi kama viongozi wa dini tukiongozwa na utashi mwema tunao uwezo wa kuondoa yanayosemwa dhidi yetu au yanayotajwa na waumini wetu bila kuomba msaada.

“Bakwata kila siku tutaendelea kuwa mstari wa mbele na kuunga mkono juhudi na harakati ambazo zinawawezesha Waislamu na Wakristo katika nchi yetu kuendelea kuishi pamoja kwa amani na usalama, tukiwa raia wa nchi moja wenye mitazamo tofauti kuhusu dini na ibada,” alisema.

Alisema BAKWATA siku zote itaendelea kuunga mkono harakati na juhudi za Serikali za kuilinda amani pamoja na kuhakikisha kuwa uhuru wa kuabudu unatumiwa vizuri.

Simba ambaye hakutaka kutaja majina ya masheikh wanaounda timu hiyo, aliwaasa wananchi kuwa watulivu wakitumia kipindi hiki kuomba dua ili Mwenyezi Mungu awaondolee mabalaa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa IPP, Reginald Mengi, amepaza sauti akisema kuwa migogoro ya dini inayotokea nchini huenda ikawa na msukumo wa kisiasa.

Mengi aliwataka wananchi kuepuka dhambi ya udini, kwani inaweza kuhatarisha amani ya nchi na watu wake ambao kwa kipindi kirefu wamekuwa wakiishi kwa umoja na mshikamano.

Mengi aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo alisema hivi sasa nchi imekuwa ikipita katika wakati mgumu, ikiwemo kushuhudia umwagaji wa damu unaotokana na kugombea haki ya kuchinja.

Mengi alisema hatua ya kugombea kuchinja imekuwa ikichafua jina la nchi katika macho ya mataifa ya nje, jambo ambalo ni aibu kwa taifa na watu wake.

“Ni aibu kubwa kwa Taifa hili la Tanzania kupigana na kumwaga damu kwa ajili ya kuchinja na ikiwa jambo hili lisipochukuliwa tahadhari mapema, kuna hatari ya hata kugombania kuchinja binadamu badala ya mnyama.

“Hili si sawa hata kidogo kuacha liendelee kutokea nchini kwetu na ni vema watu wakaelewa kuwa hata historia yetu kiutamaduni kwa muda mrefu kama wewe upo kijijini na una shughuli ambayo unaona jamii ya watu wa dini nyingine tumezoea Muislamu ndiye anayechinja mnyama.

“Na ilikuwa si ajabu kwa Mkristo binafsi kuchinja mnyama hasa pale alipokuwa akihisi kuwa mnyama huyo atakula yeye pekee, ila ilikuwa kama kuna mkusanyiko wa kijamii tulikuwa tukimtafuta Muislamu ili achinje.

“Huu ndio ulikuwa utaratibu wa enzi na enzi ambao tumeuridhia kutoka kwa mababu zetu. Nami kama Mkristo ninapenda kutoa maoni yangu haya ambayo nina imani viongozi wangu wa dini ya Kikristo wataniamini.

“Kubwa linalotakiwa kufanyika, hasa katika hili la kuchinja ni vema viongozi wa Kikristo kuwaelimisha waumini wao kuhusu utamaduni huu wa kuchinja na si Waislamu wafanye hivyo,” alisema Dk. Mengi.

Akifafanua kuhusu mizizi ya udini ambayo imeanza kuwa ajenda kwa Taifa, Mengi alisema kuwa jambo hilo huenda limekuwa na msukumo kutoka kwa wanasiasa au viongozi wa dini ambao wamekuwa na maslahi na migogoro hiyo.

“Bado tuna nafasi ya kung’oa udini na kama tukiacha uendelee, ni wazi hakuna atakayekuwa salama kupona na ikiwa tutafikia hivi sijui Watanzania watakimbilia wapi. Dhambi ya udini ni dhambi ya umauti,” alisema Dk. Mengi.

Kwa upande wake, Wassira alikemea tabia ya baadhi ya wanaocheza na amani huku akiwafananisha na wendawazimu.

Wassira alitoa kauli hiyo juzi, katika harambee ya kuchangia ujenzi wa hospital ya kisasa inayojengwa na Kanisa la Waadventista Wasabato Jimbo la Nyanza Kusini, lenye makao yake makuu Pasiansi, Jijini Mwanza.

Katika harambee hiyo, Wassira aliliomba kanisa hilo kushirikiana na madhehebu mengine nchini ili kuliombea taifa liweze kuwa na amani.

Aliwashangaa baadhi ya watu wanaotumiwa kuchochea vurugu za kidini na kuwafananisha na mtu anayekata tawi la mti alioukalia na kusema kuwa amani ikitoweka hakuna mtu atakayepona.

Kuhusu ujenzi wa hospitali hiyo, ambayo itakuwa na ghorofa tano, Wassira alisema ujenzi huo umezingatia falsafa ya waumini wa dini ya Sabato, wanaoamini duniani ni wapitaji tu.
chanzo:mtanzania
Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment