TAMPRO yamwaga misaada vijijini

Na Rashid Mtagaluka
 
JUMUIYA ya wanataaluma wa Kiislamu Tanzania Tampro imeamua kutekeleza kwa nguvu moja ya malengo ya kuanzishwa kwake kwa kuitazama zaidi jamii inayoishi vijijini, imefahamika.

Akizungumza muda mfupi kabla ya kukabidhi misaada ya nguo na chakula kwa wakazi wa vijiji tisa vya kata ya Sotele iliyoko wilayani Mkuranga mkoani Pwani, Mkurugenzi Mtendaji wa Tampro Sadik Gogo alisema wamedhamiria kuelekeza nguvu zao vijijini kwa kuwa ndiko asilimia kubwa ya Watanzania iliko.

“TAMPRO kwa kushirikiana na Shirika la kutoa misaada ya kibinaadamu na Maendeleo la Helipng Hand kutoka nchini Marekani, tumeamua kuisaidia jamii ya Watanzania hususan waishio vijijini.

“Tunafanya hivyo mbali ya kutimiza moja ya malengo tuliojiwekea wakati wa kuanzishwa kwa jumuiya hii takriban miaka 16 iliyopita, lakini pia ni kuitikia wito wa serikali wa kusaidiana nayo katika kuharakisha maendeleo ya Watanzania”, alisema Gogo.

Aidha Mkurugenzi huyo Mtendaji wa Tampro alisema pamoja na kaya zipatazo 2700 kutoka katika vijiji hivyo tisa vya kata ya Sotele kunufaika na msaada wa nguo na vyakula, pia msaada kama huo wameutoa katika vijiji vitatu vilivyoko kata ya Mkamba wilayani Rufiji mkoani Pwani.

“Vilevile zoezi hili tumekwishalifanya katika mikoa ya Mara, Ruvuma na Mwagwepande mkoani Dar es Salaam ambako watu walioathirika na mafuriko walikuwa wakihitaji misaada hiyo”, aliongeza Gogo.

Kwa upande wake Mratibu mkuu wa Helpin Hand Sajid Iqbal ameliambia KISIWA kuwa, tokea mwaka 2012 Shirika lake limefanikiwa kuisaidia jamii ya Watanzania kwa kushirikiana na marafiki zao hao wa TAMPRO.

“Japokuwa Heliping Hand ni shirika la misaada lenye makao makuu yake nchini Marekani, lakini takriban nchi nane za Afrika ikiwemo Tanzania mpaka sasa zimefaidika na misaada tunayoitoa”, alisema Iqbal.

Baadhi ya nchi nyingine ambazo shirika hilo limekuwa zikitoa misaada ya Elimu, Afya, Vyakula, mavazi na uchimaji wa visima vya maji safi ni pamoja na Kenya, Somalia, Uganda, Libya, Mali, Sudan na Ethiopia.

Nao baadhi ya wakazi wa kijijini hapo wamelishukuru shirika hilo kwa upande wa kwanza, lakini wameishukuru TAMPRO kwa upande mwingine kwa uamuzi wao wa kuelekeza misaada hiyo vijijini hususan hapo Sotele.

Mwisho wametoa wito kwa asasi nyinginezo nchini kuiga mwenendo na utendaji kazi wa wanataaluma hao wa Kiislamu Tanzania ambao bila ya shaka wamedai utawapelekea kwenye mafanikio.
Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment