Harufu ya kuisha kwa mgogoro baina ya Zitto Kabwe na
chama chake cha Chadema inanukia, lakini mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini
anataka kuwapo na mazungumzo kubaini tatizo ili atakayebainika kuwa alifanya
makosa awe tayari kuomba radhi hadharani.
Zitto alikiri bungeni kuwa amekuwa “akimiss” harakati
zilizokuwa zikifanywa na vyama vya upinzani wakati wa Bunge Maalumu la Katiba,
harakati zilizozaa Umoja wa Katiba ya Wananchi na kufurahia kuhudhuria kwa mara
ya kwanza vikao vya umoja huo.
Zitto, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu
za Serikali (PAC), alipata fursa ya kuingia vikao vya Ukawa wakati wapinzani
walipoungana tena kupambana dhidi ya wizi wa fedha kutoka Akaunti ya Tegeta
Escrow, sakata ambalo liliwekwa bayana na kamati yake baada ya Mbunge wa Kigoma
Kusini, David Kafulila kulifikisha bungeni, lakini hakudokeza lolote kuhusu
Chadema.
Hata hivyo, mapema wiki hii, Zitto, ambaye Novemba mwaka
jana alivuliwa nyadhifa zote kwenye chama hicho kwa tuhuma za kukihujumu,
lakini akafanikiwa kulinda uanachama wake baada ya kufungua kesi mahakamani na
kufanikiwa kupata amri ya kuzuia asijadiliwe.
Baada ya kuongoza PAC kuchunguza wa tuhuma za Escrow na
kufanikiwa kulishawishi Bunge kufikia maazimio manane ya kuwashughulikia
kisheria wahusika kwenye uchotwaji huo wa fedha, kumekuwapo na wito kutoka kwa
baadhi ya wafuasi wa Chadema kutaka pande hizo mbili zimalizane.
“Kabla ya jambo lolote kufanyika, ili kukata kiu ya
Watanzania wanaotaka kuona tunaondoa tofauti zetu, ni lazima kusema ukweli na
kila upande kuwa tayari kuomba radhi hadharani pindi ikibainika ulifanya
makosa,” alisema Zitto alipotakiwa kuzungumzia harakati hizo za kumrejesha
Chadema.
“Ukweli wangu ndani ya Chadema ni nini? Lakini mimi
ninaona sina kosa ndani ya Chadema. Ninachotaka mimi nielezwe ukweli bila
chembe ya shaka makosa yangu mimi ni nini,” alisema na kuongeza:
“Nitakuwa tayari kuomba radhi hadharani kama ikibainika
nilifanya makosa na kama ikibainika chama kilifanya makosa, nacho kiwe tayari
kuomba radhi hadharani na ukweli uwe mbele katika maridhiano.
“Kama hakutakuwa na ukweli itakuwa vigumu kupata
mwafaka. Mimi sina tatizo. Nirudie nilivyosema bungeni kuwa nina-miss sana
(ninapenda sana kuwamo kwenye) harakati za mageuzi kipindi hiki za kuiondoa CCM
madarakani.”
Katika mkutano na waandishi wa habari mara baada ya
kuvuliwa nyadhifa zote, Zitto alisema: “Natambua kuwa wapo ambao wangependa
kutumia nafasi zao kudhoofisha mapambano ya siasa za demokrasia nchini mwetu.
Napenda wanachama wa Chadema na wapenda demokrasia watambue kuwa, mimi bado ni
mwanachama mwaminifu wa chama hiki.
“Kinachoendelea ndani ya chama chetu ni mapambano ya
kukuza demokrasia. Ni mapambano baina ya wapenda demokrasia dhidi ya
wahafidhina; waumini wa uwajibikaji dhidi ya wabadhirifu; na wapenda siasa safi
dhidi ya watukuzao siasa majitaka.”
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, ambaye binafsi
aliguswa na mzozo huo, hakuwa tayari kuzungumzia kumaliza matatizo baina ya
chama na Zitto.
“No comment (sina maoni) kwa hilo. Siwezi kuzungumzia
suala hili katika media (vyombo vya habari),” alisema Mbowe
Hoja ya kutaka Zitto arejeshwe Chadema imekuwa ikisambaa
katika mitandao ya kijamii na kwa baadhi ya wanasiasa baada ya kuonekana kuwa
karibu na viongozi wa chama chake wakati Kamati ya PAC ilipoibua ufisadi wa
Sh306 bilioni kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow wiki iliyopita.
Wakati akihitimisha mjadala wa sakata la Escrow, mbali
na kueleza bayana kuwa alifurahia kuhudhuria vikao vya Ukawa kwa mara ya
kwanza, Zitto alikwenda mbali na kumpongeza “kwa namna ya pekee” Mbowe kwa
jinsi walivyoshirikiana katika sakata hilo.
Zitto alisema hilo lilikuwa ni jambo la kitaifa ndiyo
maana wabunge wote wa upinzani bila kujali vyama vyao waliungana.
Alisema mara baada ya sakata hilo kumalizika watu
mbalimbali wamekuwa wakizungumzia kufanyika kwa maridhiano ili awe sehemu ya
Ukawa na kwamba haoni tatizo.
“Katika hili, kipekee namshukuru kiongozi wa Kambi Rasmi
ya Upinzani kwa kuniunga mkono katika sakata hili,” alisema Zitto.
Kuhusu taarifa za kujiunga kwake na chama kipya cha
ACT-Tanzania alisema: “Hizo ni taarifa ambazo hazina ukweli wowote.”
Kuhusu kesi aliyofungua mahakamani dhidi ya Chadema,
Zitto alisema:
“Nilifungua kesi kwa sababu ya kulinda uanachama wangu,
lakini mazungumzo yakifanyika na kujua kosa langu ni nini, nitaifuta kesi hiyo
na kuanza upya harakati.”
CHANZO: Forumhuru.com

0 comments:
Post a Comment