SERIKALI imekubali kutopandisha ushuru wa petroli na dizeli na kupunguza ushuru wa mafuta ya taa. Hatua hiyo ilielezwa bungeni jana na Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa alipokuwa akihitimisha mjadala wa Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2013. Muswada huo, unahusu marekebisho ya sheria mbalimbali 22 katika ushuru, kodi na tozo.
Alisema ushuru wa petroli, utabaki katika kiwango cha sasa cha Sh 339 kwa lita na dizeli Sh 215 kwa lita, wakati ushuru wa mafuta ya taa utashuka kutoka Sh 430 hadi Sh 425 kwa lita.
Wakati akiwasilisha Bajeti ya Serikali ya mwaka 2013/14 Juni 13, mwaka huu, Waziri Mgimwa alipendekeza ushuru wa petroli upande kutoka Sh 339 kwa lita hadi Sh 400 kwa lita, dizeli kutoka Sh 215 hadi Sh 217 na mafuta ya taa ushuru ubaki Sh 400.30 kwa lita.
Alisema Serikali imechukua hatua ya kutoongeza ushuru kwenye petroli na dizeli, kuepuka mfumuko wa bei, uchakachuaji na kudumisha biashara nzuri na nchi jirani.
Kupandishwa kwa ushuru wa petroli na dizeli, kulisababisha malalamiko makubwa kutoka kwa wabunge kwamba kungesababisha kupanda kwa mfumuko wa bei na kuleta hali ngumu ya maisha kwa wananchi wengi.
Alisema tozo ya petroli kwa ajili ya mfuko wa barabara, itabaki kama ilivyokuwa awali (ongezeko la Sh 63 kwa maana ya kutoka Sh 200 hadi Sh 263).
Hivyo hivyo, kwa tozo ya dizeli kwa ajili ya ukarabati wa barabara za vijijini, itaongezeka kutoka Sh 200 hadi Sh 263.
Kuhusu simu za mkononi alisema kodi iliyowekwa haitahusisha kutuma na kupokea fedha kwa kutumia simu hizo.
Suala hilo, nalo lililalamikiwa kwa kiasi kikubwa na wabunge ambao walisema kodi hiyo ingewaathiri mno wananchi hasa wa vijijini wanaotumia huduma hiyo na ambao ni vigumu kupata huduma za benki.
Pia alizungumzia msamaha wa kodi ya zuio kwa ukodishaji wa ndege kutoka nje ambayo alikuwa amependekeza uondolewe.
Alisema msamaha huo, hautaondolewa sasa bali hatua hiyo itatekelezwa kuanzia Julai mwaka 2014, kutoa fursa ya kufanya maandalizi ya kutosha.
Awali, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Andrew Chenge alisema kamati yake ilikutana na waziri na wasaidizi wake hadi saa 6.00 usiku juzi, kujadili mapendekezo ya marekebisho mbalimbali yaliyokuwa yamewasilishwa na wabunge pamoja na ya kamati yenyewe.
Chenge ambaye pia ni Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), alisema baadhi ya marekebisho hayo yalikataliwa na mengine yalikubaliwa hadi ulipofikiwa mwafaka.
0 comments:
Post a Comment