'Mafuriko kutikisa hadi Mei'

Moja ya sehemu zilizokumbwa na mafuriko Jijini Dar es Salaam
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imesema mvua zinazoendelea kunyesha zinaweza kuleta athari kubwa zaidi katika maeneo ya bondeni. Mamlaka hiyo, imesema msimu huu huwa na kiwango kikubwa cha mvua ukilinganisha na miezi ya Oktoba, Novemba na Desemba.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Agnes Kijazi alisema kuna kila sababu ya wananchi wanaoishi mabondeni kuondoka kutokana na kiwango cha mvua kinachotegemewa kutokea.

Alisema mvua hizo, zinaweza kuleta athari kubwa zaidi katika maeneo ya bondeni, kwani msimu huu huwa na kiwango kikubwa cha mvua ukilinganisha na miezi ya Oktoba, Novemba na Desemba.

“Kwa sasa siwezi kutoa jumla ya kiwango cha mvua zote zinazoendelea kunyesha hadi msimu huu utakapomalizika, tutajumlisha na tutapata wastani wa mvua zote zilizonyesha nchini.

“Ingawa katika baadhi ya vituo vyetu, wameweza kutoa viwango vya mvua iliyonyesha jana na kiwango kikubwa zaidi ni kile cha milimita 140.7 katika kituo cha Mafia,” alisema Kijazi.

Alisema kwa wakazi wanaoishi karibu na mitaro ya maji, wapo kwenye hatari ya kukumbwa na mafuriko, kwani mingi imeziba na kujaa michanga, hali inayopelekea maji mengi kuenea kwenye makazi yao.

“Mvua za msimu huu ni za vipindi vya muda mfupi na mrefu, kuna wakati mwingine jua litawaka na mvua zikiendelea kunyesha kubwa hivyo kutokana na ardhi kushiba maji ni rahisi kutokea kwa mafuriko.

“Kwa maeneo ya Pwani, kutakuwa na matarajio ya mvua nyingi kwa kipindi hiki kuanzia leo (jana) hadi mwisho wa Machi ambazo zitakuwa ni za kawaida,” alisema Kijazi.

Pia aliwataka wananchi wawe na tabia ya kufuatilia utabiri wa hali ya hewa kila unapotolewa na mamlaka hiyo, ili kuweza kujiandaa na mabadiliko yanayotokea pia kujua uelekeo wa mvua zinazonyesha nchini.

“Wakazi wanaoishi maeneo ya mabondeni mnatakiwa kuchukua tahadhari mapema kwa kuhama, kwani mvua zinazoendelea kunyesha zimesababisha kuwa na maji mengi zaidi ukilinganisha na mwaka jana,” alisema Kijazi.

WAKAZI WALALAMIKA

Wakati huo huo, wakazi wa Magomeni na Jangwani mjini Dar es Salaam, wamelalamikia ujenzi unaoendelea wa mradi wa ujenzi wa barabara ya mabasi yaendayo kasi (DART), kuwa chanzo cha mafuriko kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha.

Wakizungumza na MTANZANIA jana, wakazi hao wameelezea kuwa ujenzi huo umeziba miundombinu ya mikondo ya maji ambayo ilisababisha mvua iliyonyesha juzi maji kuingia ndani hivyo kuleta usumbufu kwa wakazi hao.

Mmoja wa wakazi hao, Fatuma Rashid alisema mvua hiyo imesababisha mashimo karibu na makazi ya watu.

Taarifa hii, imeandaliwa na Agatha Charles na Charles Kulaya, Oliver Oswald na Maneno Selanyika, Dar es Salaam
 chanzo:mtanzania

Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment