JAMHURI YA AFRIKA YA KATI: WAASI WANAZIDI KUSONGA MBELE, WAUTWAA MJI MUHIMU

Rebels of the Seleka coalition in CAR patrol on a road 12 kilometers from the city of Damar on January 10, 2013.
Waasi wa Seleka wakifanya ulinzi umbali wa kilometa 12 kutoka mji wa Damara, Januari 10, 2013





Waasi katika Jamhuri ya Afrika ya Kati wamesonga mbele kuelekea mji mkuu wa nchi hiyo Bangui na wameutwaa mji muhimu wa jirani.

Shirika la habari la AP liliripoti kuwa jana Ijumaa, waasi wa Seleka waliuchukua mji wa Damara, ulio kilometa 68 (maili 42) katika mkoa wa kaskazini wa Ombella-M'Poko.  

Kwa kuutwaa mji wa Damara, waasi wamevuka msitari uliowekwa na vikosi vya kanda hiyo mwezi januari.

Mapema siku hiyo, vikosi vya waasi viliushambulia mji wa Bossangoa, uliopo kilometa 303 (maili188) kaskazini mwa Bangui.

"Bossangoa imechukuliwa bila upinzani. Na kama ujuavyo, Bossangoa ni ngome ya Rais Francois Bozize. Tuliichukua Bossangoa asubuhi na mpaka mchana wanajeshi wetu walikuwa Damara," msemaji wa Seleka, Eric Massi alisema kwa njia ya simu.

Vile Massi aliongeza kuwa waasi walikuwa wameanza kupenya kwa siri kuelekea mji mkuu.

"Sasa hivi wanaelekea mji mkuu…tunatoa wito kwa wananchi na askari waweke silaha zao chini. Na tunawataka wanajeshi wetu wathibitishe kuwa wana nidhamu, waache uporaji ili kuepuka mapigano yasiyokuwa ya lazima,” alisema msemaji huyo wa waasi.

Wakati huo huo, hofu imetenda mjini Bangui na wakazi wengi walio upande wa kaskazini wa mji huo wameondoka.

Vilevile, jana Ijumaa, Mwendesha mashitaka wa Mahakama ya Kimataifa ya makosa yajinai (ICC), Fatou Bensouda, alielezea wasiwasi wake kuhusu hali inavyoendelea katika nchi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati.

"Nimehuzunishwa sana na ripoti za hali mbaya nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, na tuhuma za uhalifu mkubwa katika mgogoro unaoendelea sasa,” Bensouda alisema na kuongeza, "Ninazikumbusha pande zote zinazohusika na mgogoro huo kuwa ICC ina mamlaka ya kisheria nchini humo na ofisi yangu haitasita kufanya uchunguzi na kuwashitaki wote wanaotuhumiwa kufanya uhalifu huu.”

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipanga kufanya kikao cha ndani cha dharura kujadili matukio yanayoendelea katika nchi hiyo.

Siku ya Alhamisi, waasi wa muungano wa seleka waliitwaa miji miwili kaskazini mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Waasi hao walianza kuuteka mji wa Bouca, wenye uwanja wa ndege unaopatikana kiasi cha kilometa 300 (maili 240) kaskazini mwa mji mkuu Bangui,  na kisha wakautwaa mji wa Batangafo, kilometa 100 (maili 62) kaskazini.

Siku ya Jumatano, televisheni ya serikali ilitangaza matangazo mawili ya rais ya kuwaacha huru wafungwa wa kisiasa, kuondosha hali ya hatari na kuondosha vikwazo vya barabarani vinavyolindwa na wapiganaji wanaomtii Bozize.

"Htuna imani tena na ahadi za Bozize. Tunamtaka ajiuzulu, vinginevyo tunamuondosha kwa nguvu," msemaji wa Seleka alisema kwa njia ya simu siku ya Alhamisi.

Massi aliongeza kusema kuwa wapiganaji wa Seleka walikutana na upinzani mdogo kutoka kwa vikosi vya serikali mjini Bouca, na walifanikiwa kuwakamata wanajeshi watatu wa serikali na magari mawili ya kijeshi.

Siku ya Jumatano, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilielezea "wasiwasi mkubwa" kuhusu kuibuka kwa mgogoro nchini humo katika taarifa iliyosomwa na Rais wa Baraza la Usalama, Vitaly Churkin katika mkutano na vyombo vya habari.

Mnamo Januari 11, rais wa nchi hiyo na wawakilishi wa waasi waliasaini makubaliano mjini  Libreville, Gabon baada ya siku tatu za mazungumzo yaliyosimamiwa na nchi jirani.

Chini ya makubaliano hayo, baadhi ya viongozi wa upinzani na wanachama wa muungano wa Seleka walipewa nyadhifa kadhaa muhimu katika serikali.

Waasi wamekuwa wakiituhumu serikali kutotekeleza makubaliano hayo, na wametaka kuachiwa huru kwa wafungwa wao.

Waasi wa Seleka walianza hujuma dhidi ya serikali mwezi Desemba 2012.

Jamhuri ya Afrika ya Kati ina utajiri mkubwa wa maliasili za madini kama vile dhahabu na almasi. Lakini, kama ilivyo kwa nchi nyingi za Kiafrika, nchi hiyo inakabiliwa na umaskini wa kutisha na imekumbwa na mlolongo wa uasi na mapinduzi tangu ilipopata uhuru mwaka 1960.

Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment