INTANETI YAZIMIKA NCHI NZIMA


Imeelezwa kuwa tatizo kukosekana kwa mtandao wa intaneti nchi nzima jana limetokana na kukatika kwa mikongo miwili ya mawasiliano ya taifa.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simu Tanzania (TTCL), Dk Kamugisha Kazaura alisema Tanzania inaunganishwa na mikongo miwili ya mawasiliano ya Easy na Seacom ambayo yote imekatika na hivyo kusababisha tatizo hilo.

Dk Kazaura alisema Mkongo wa Easy umekatika nchini Misri, kilometa 17  na 19 katika Bahari ya Mediterranean huku Mkongo wa Seacom ukiwa umekatikia Marseille nchini Ufaransa.

“Tunajaribu kufanya juhudi za kuona namna gani tunaweza kufanya ili kuendelea kupata mtandao, tumewasiliana na wadau wa Seacom ambao wametuahidi kutupa kiasi cha 1.24 kwa sekunde,” alisema Dk Kazaura.

Alisema watu wa Seacom walisema kuwa matengenezo ya Mkongo huo yanaweza kuchukua muda wa wiki mbili ili kukamilika. Lakini watu wa Easy hawajasema ni muda gani mpaka matengenezo kukamilika.

“Seacom wanajaribu kuangalia njia nyingine kama kuna uwezekano wa kupewa masafa mengine mpaka hapo matengenezo ya Mkongo yatakapokamilika,” alisema.

Hata hivyo, alisema mabenki hayataweza kuathirika na hali hiyo kutokana na wao kuwa na mfumo ambao unawezesha kuendelea na shughuli zao.

Tatizo la ukosefu wa mtandao wa intaneti jana liliathiri taasisi nyingi za hapa nchini zinazotumia mtandao unaotokana na Mkongo wa Mawasiliano wa Taifa.

CHANZO: HABARILEO
Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment