Katika kuchukua hatua za kukabiliana na uhalifu nchini, serikali
kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi inakamilisha mazungumzo na baadhi ya
makampuni ili kuweka kamera maalumu za ulinzi katika miji mbalimbali nchini.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe, aliliambia
Bunge jana kuwa wizara yake ilikuwa ikifanya mazungumzo na makampuni makubwa
kuhusu suala hilo na kwamba hivi karibuni kamera hizo za CCTV zitaanza
kutumika.
Alisema hatua hizo zinachukuliwa kufuatia ongezeko la
matukio ya uhalifu katika miji mikubwa kama vile Dar es Salaam, Arusha, Mwanza
na Zanzibar. “Tunafanya mazungumzo na makampuni madhubuti kuhusu mfumo wa
uchunguzi… tunatarajia kuanza kutekeleza mradi huu muda si mrefu,” alisema
Waziri Chikawe.
Alisema tahthmini ya awali imeshafanyika katika miji ya Dar
es Salaam na Zanzibar na kwamba utekelezaji
utaaza hivi karibuni.
Kwa mujibu wa waziri huyo, baada ya kuweka mfumo huo Dar
es Salaam na Zanzibar, mradi huo
utaendelea kwenye miji mingine mikubwa nchini.
“Hili ni suala la kawaida kwa malengo ya ulinzi…
tutaanza na Dar es Salaam na Zanzibar na baadaye tutaelekea kwenye maeneo
mengine,” alisema.
Waziri Chikawe alikuwa akimjibu mbunge wa Mwibara (CCM)
mheshimiwa Kangi Lugola aliyetaka kujua ni lini serikali itaweka kamera za CCTV
katika miji ya Dar es Salaam, Mwanza, Tanga, Moshi, Morogoro, Mbeya na Arusha.
Mheshimiwa Kangi Lugola alieleza kuwa
miji hiyo imekuwa na matukio mengi ya uhalifu na kwamba kuna haja kwa serikali
kutumia teknolojia ya kisasa kukabiliana na hali hiyo.
Aidha, bwana Lugola alipingana na serikali kuruhusu
makampuni binafsi kuweka kamera za CCTV, akisema masuala yanayohusu usalama wa
taifa yanatakiwa kupewa kipaumbele.
“Tumebinafsisha kila kitu; makampuni, mshamba na mali
nyingine nyingi za umma… leo tunazungumzia makapuni binafsi kuweka kamera za CCTV…
serikali inatakiwa kuwa makini jinsi inavyolishughulikia suala hili,” alisema.
Hata hivyo, waziri Chikawe alisema kuwa serikali iko
makini na imejizatiti kuhakikisha ulinzi na usalama wa wananchi na mali zao.
Akizungumzia hatua zinazochukuliwa kukabiliana na ajali
za barabarani, naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa
Pereira Silima alisema kuwa serikali inakamilisha mpango wa kuweka mfumo
maalumu wa kufuatilia magari.
CHANZO: The Citizen
0 comments:
Post a Comment