Wiki moja kabla ya kusitishwa huduma za programu ya
kompyuta (OS) ya Windows Xp, imefahamika kuwa waathirika wakubwa watakuwa ni
benki na taasisi za fedha ambazo hutumia mfumo huo katika mashine za kutolea
fedha (ATMs)
Shirika la Microsoft limethibitisha kuwa benki ni
miongoni mwa taasisi nyingi zitakazoathirika na mabadiliko hayo.
Baadhi zimeanza kufanyia kazi tatizo hilo, ikiwamo benki
moja ambayo jana alasiri ilituma ujumbe kwa wateja wake kuwa, “Ndugu mteja,
kuanzia Jumamosi saa 2:00 usiku Aprili 5, mpaka Jumapili saa 12:00 asubuhi
tutakuwa tunaboresha mashine zetu za ATM, hivyo kadi yako haitafanya kazi kwa
kipindi hiki. Asante.”
Kwa mujibu wa Microsoft asilimia kubwa ya benki katika
nchi zinazoendelea zinatumia programu ya Windows XP katika kuendesha ATM, hivyo
kuwa moja ya waathirika wa mpango huo.
Katikati ya Machi, Microsoft ilitangaza kusitisha huduma
zote zinazohusiana na bidhaa zake za Windows Xp kufikia Aprili 8, mwaka huu.
Pia shirika hilo litasitisha ufanisi wa programu ya kuzuia na kupambana na
virusi ya Microsft Security Essentials katika mfumo wa Windows Xp, hivyo
kufanya urahisi wa kompyuta zinazoitumia kukosa ulinzi.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Twiga Hosting, Jacob Urassa
alisema Watanzania hawatakiwi kupuuza onyo hilo kwa kuwa ikifika Aprili 9
usalama wa taarifa zao utakuwa hatarini.
“Windows XP ni dhaifu mara tano zaidi ya Windows 7 na 8,
kwa hiyo Microsoft wameona ni bora wakaitoa sokoni. Kwa maana hiyo ATM na
kompyuta zote zinazotumia programu hizo hazitakuwa na ulinzi wa uhakika,”
alisema Urassa ambaye ni mtaalamu wa masuala ya Teknolojia ya Mawasiliano (IT).
Alisema kuwa kuna idadi kubwa sana ya Watanzania
wanaoendelea kutumia bidhaa hizo zikiwemo taasisi kubwa nchini hivyo kuna haja
kubwa ya kuchukua hatua za kubadilika na teknolojia.
Naye, Ofisa Uhusiano wa Benki ya Posta, Noves Moses
aliwatoa wasiwasi wateja wake kuwa licha ya kusitishwa kwa matumizi ya Windows
XP, bado benki hiyo itaendelea kutoa huduma zenye kiwango kile kile.
CHANZO: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment