MKAZI wa Mtaa wa Uhamila katika mji mdogo wa Rujewa,
mkoani Mbeya, amehukumiwa miaka 65 jela kutokana na makosa matatu tofauti, yaliyotokana
na kumpa ujauzito mwanawe wa kumzaa.
Mahakama ya Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya ilitoa hukumu
hiyo jana kwa Benjamin Muyinga (48) baada ya kutiwa hatiani kwa makosa hayo.
Hakimu Mfawidhi Kinabo Minja alimhukumu mshitakiwa kutumikia
jela miaka 30 kwa kosa la kufanya mapenzi na mtoto wake, miaka 30 mingine kwa
kubaka mtoto wake na miaka mitano jela kwa kumpa mimba mwanafunzi.
Minja alisema ameridhishwa na ushahidi uliotolewa
mahakamani hapo hivyo atatumikia adhabu hiyo kwa pamoja kwa maana kwamba atakaa
jela miaka 30.
Mashitaka yaliyokuwa yakimkabili mahakamani hapo ni
kufanya mapenzi na mtoto wake, kubaka mtoto wake na la tatu ni kumpa mimba
mwanafunzi.
Awali ilidaiwa mahakamani na Mwendesha Mashitaka wa
jeshi la Polisi, Mazoya Luchagula, mbele ya Hakimu Mfawidhi Kinabo Minja,
Oktoba 18 mwaka jana, mwanafunzi (jina linahifadhiwa) aliyekuwa na umri wa
miaka 14, alikuwa mjamzito.
Luchagula alidai walimu wa shule hiyo ndiyo walitilia
shaka suala la mwanafunzi huyo aliyekuwa darasa la tano katika shule ya msingi
iliyoko Rujewa kwamba alikuwa na ujauzito. Alipelekwa hospitali na kwenda
kukutwa akiwa na mimba ya miezi minne.
Kwa mujibu wa Mwendesha Mashitaka, baada ya kuhojiwa,
mwanafunzi huyo alidai ujauzito ulikuwa wa baba yake mzazi waliyekuwa wakiishi
naye wawili nyumbani kutokana na baba yake kutengana na aliyekuwa mkewe ambaye
hivi sasa anaishi jijini Mbeya.
Mwanafunzi huyo alibainisha namna alivyokuwa akiishi na
baba yake baada ya wazazi wake kutengana na kwamba alimgeuza ‘mkewe’ kwani
alikuwa akilala naye na kufanya naye mapenzi hadi ilipobainika kuwa na ujauzito
huo.
Katika kile kilichoelezwa na upande wa mashitaka kwamba
kitendo kilichofanywa na mzazi huyo hakikubaliki katika jamii ya Watanzania,
Mwendesha Mashitaka aliomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mshitakiwa iwe
fundisho kwake na wazazi wengine wenye tamaa zenye kusababisha ukatili dhidi ya
watoto wao.
0 comments:
Post a Comment